Marekani na Umoja wa Afrika zalaani ukandamizaji Sudan
20 Novemba 2021Marekani na Umoja wa Afrika zimelaani vitendo vya kuwakandamiza waandamanaji na ziwataka viongozi wa Sudan kuacha matumizi ya nguvu dhidi ya raia.
Kwa mujibu wa madaktari, wengi wa waliouawa katika maandamano yaliyofanyika siku ya Jumatano walikuwa ni watu kutoka Kaskazini mwa mji mkuu wa Sudan, Khartoum, ng'ambo ya Mto Nile.
Leo Jumamosi, makumi ya watu walikusanyika kuadhimisha vifo vya waandamanji wenzao waliouawa huko kaskazini ya Khartoum. Waandamanaji hao waliimba nyimbo zilizohimiza kulipiza kisasi na kuwataka viongozi wa kijeshi kupisha utawala wa kiraia.
Chama cha wanataaluma kimesema SPA vikosi vya usalama vilivamia makazi ya watu na misikiti hapo siku ya Ijumaa na kimetoa wito wa wale waliohusika na ukiukaji wa haki za binadamu pamoja na matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji waliokuwa wanaandamana kwa amani, wawajibishwe.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Ned Price ametoa wito kwa mamlaka za Sudan ziruhusu maandamano ya amani yafanyike.
Hata hivyo maafisa wa polisi wanakanusha kutumia risasi za moto na wamesisitiza kuwa wametumia nguvu ndogo tu kuwatawanya watu walishiriki katika maandamano hayo.
Chama hicho cha wanataaluma wa Sudan SPA, kimewataka raia kuendeleza kampeni ya kuunga mkono maandamano. SPA ni mwamvuli wa vyama vilivyoongoza maandamano ya miezi kadhaa yaliyosababisha rais Omar al Bashir kuondolewa madarakani mwaka 2019.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat amezitaka mamlaka za Sudan kurejesha utaratibu wa kikatiba na kipindi cha mpito cha kidemokrasia kulingana na makubaliano ya mwaka 2019 yanayozingatia kugawana madaraka kati ya jeshi na raia.
Wakati huo huo kamati ya kuwalinda waandishi wa habari imetoa wito wa kuachiwa waandishi wa habari waliokamatwa wakati walipokuwa wanaripoti juu ya maandamano ya kupinga mapinduzi.
Sudan ina historia ndefu ya mapinduzi ya kijeshi, ikifurahia kwa nadra tu utawala wa kidemokrasia tangu ilipopata uhuru mnamo mwaka 1956.
Chanzo:/AFP