Stoltenberg: NATO kufanya maamuzi muhimu kuhusu Ukraine
18 Juni 2024Rais wa Marekani Joe Biden amefanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami, NATO Jens Stoltenberg siku ya Jumatatu.
Baada ya mkutano huo, Stoletenberg aliwaambia waandishi wa habari kwamba, alikuwa na mazungumzo mazuri na Biden na walijadiliana juu ya mkutano ujao wa kilele wa NATO mjini Washington DC, mnamo mwezi Julai.
"Tulijadiliana juu ya mkutano ujao wa kilele wa NATO hapa Washington mwezi ujao, ambapo tutakuwa tunasherehekea miaka 75 ya mafanikio makubwa katika historia ya muungano huu, lakini pia ni mahali ambapo huwa tunafanya maamuzi muhimu kwa ajili ya siku za usoni na hasa matumizi ya ulinzi. Lakini pia tutafanya maamuzi muhimu juu ya Ukraine," amesema Jens Stoltenberg.
Stoltenberg aidha ametangaza kwamba zaidi ya washirika 20 wa NATO watatumia asilimia 2 ya pato jumla la ndani katika bajeti ya ulinzi kwa mwaka huu.