Stoltenberg asema NATO ingeweza kuisaidia zaidi Ukraine
14 Septemba 2024Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg, amesema katika mahojiano kwamba muungano huo wa kijeshi ungeliweza kujaribu kuzuia uvamizi wa Urusi mwaka 2022.
Stoltenberg, ambaye anamaliza muda wake wa kuiongoza jumuiya hiyo, ameweka wazi kwamba NATO ilisita kufanya maamuzi ya kutoa silaha ambazo Ukraine iliomba kabla ya uvamizi kamili wa Urusi kwa kuhofia kwamba mvutano baina yao na Urusi ungeongezeka maradufu.
Soma zaidi. Je, NATO inapaswa kudungua droni za Urusi?
Katika mahojiano hayo yaliyochapishwa leo na gazeti la kila siku la Ujerumani la FAS, Jens amesema kwa sasa nchi za NATO zinatoa msaada wa vifaa vya kijeshi kuisaidia Ukraine na kuzuia vita.
Alipoulizwa kuhusu mwisho wa vita, Stoltenberg alisema ikiwa Ukraine itashinda basi hatua hiyo itakuwa mafanikio katika meza ya mazungumzo na Urusi, lakini hilo linategemea nguvu za Ukraine katika uwanja wa mapambano.