Steinmeier ampongeza Macron kwa kuimarisha ushirikiano Ulaya
28 Mei 2024Akizungumza mjini Muenster ambako rais Macron amepewa tuzo ya kimataifa ya amani ya Westphalia, kwa juhudi zake za kuimarisha ushirikiano wa bara la Ulaya, rais wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier amemwambia Macron kwamba ni mchapa kazi na mtu wa kutia moyo. Steinmeier amesema wakati viongozi wengine wanapozungumzia mipaka Macron anazungumzia upeo wa macho.
Rais huyo wa Ujerumani ameendelea kusema anaamini ukweli kwamba Ufaransa na Ujerumani zimekaribiana sana katika nyakati za sasa kutokana na juhudi pia za Macron, ambaye amemueleza kama kiongozi anayekuwa tayari kila wakati kuijongelea Ujerumani, kuanzisha mazungumzoi na kujaribu kuwashawishi Wajerumani na kujaribu kuwatoa kutoka maeneo kadha wa kadha ambako huwa wanajificha.
Soma pia: Macron aupongeza ushirikiano wa Ufaransa na Ujerumani
Macron ameelezea matumaini yake kwamba uhusiano kati ya Ufaransa na Ujerumaniunaweza kuwatia moyo na kuwahamasisha wengine wengi. Macron akasema, "Ufunguo ni kwamba lazima tuzingatie uhusiano kati ya Ufaransa na Ujerumani linapokuja suala la ulinzi kwa sababu ulinzi huu sio tena dhidi yetu. Ni jukumu la pamoja kuvikabili vitisho vya pamoja. Hilo ndilo jambo muhimu linalopewa uzito katika mapinduzi ya wakati huu tulionao. Inahusu Ulaya ambayo kwa msingi ywke inatafakari kuhusu amani na usalama."
Macron ahimiza amani na usalama Ulaya
Rais Macron pia amesema bara la Ulaya lenye amani na usalama ina maana Ulaya iliyoungana pamoja na Ujerumani na Ufaransa inayofanya kazi pamoja kwa kushirikiana kupambana na vitisho vya pamoja.
Steinmeier amezingatia kwa makini wito wa Macron wa kutaka pawepo sera ya pamoja ya usalama ya Ulaya, ulinzi na hatua za pamoja kuhusu usalama wa ndani.
Macron na mke wake Brigitte, rais Steinmeier na rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, wamesaini kitabu cha dhahabu cha mji wa Muenster baada ya sherehe ya utoaji tuzo ya kimataifa ya amani ya Westphalia.
Macron amepewa tuzo hiyo ya amani ya kimataif aya Westphalia siku ya tatu na ya mwisho ya ziara yake ya kiserikali nchini Ujerumani, kabla mazungumzo na kansela Olaf Scholz yatakayotuwama juu ya sera ya ushindani barani Ulaya na ushirikiano katika masuala ya ulinzi.
Mahusiano kati ya Ufaransa na Ujerumani yamekabiliwa na msuguano katika kipindi cha miaka miwili ya utawala wa serikali ya Scholz, huku tofauti zikijitokeza kuhusu Ukraine na mafungamano ya kiuchumi na Marekani na China.
(dpa)