Steinmeier ahimiza ushirikiano wa kimataifa
21 Novemba 2018Cyril Ramaphosa ameyasema hayo jana (20.11.2018)mjini Cape Town wakati rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akimaliza ziara yake ya siku tatu nchini humo.
Ramaphosa alisema Ujerumani ni mshirika mkubwa wa tatu duniani wa kibiashara wa Afrika kusini na ni mmoja kati ya wawekezaji wakubwa wa kigeni katika nchi hiyo. Amesema zaidi ya makampuni 600 ya Ujerumani yanafanyakazi nchini Afrika kusini, ambapo yameweza kutengeneza nafasi zaidi ya laki moja za kazi.
"Kama ilivyoonekana katika mazungumzo yetu na viongozi wa makampuni ya Ujerumani mjini Berlin mwezi uliopita, Afrika kusini inaonekana kuwa sehemu muhimu ya uwekezaji. Na kuna hamasa kubwa kwa makampuni ya Ujerumani kupanua uwapo wao hapa."
Ujerumani na Afrika kusini zitakuwa wanachama ambao si wa kudumu katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2019 na 2020 na rais Cyril Ramaphosa amesema wamekubaliana kwamba nchi zao zitafanyakazi kwa pamoja kuhimiza amani ya dunia na usalama pamoja na kuimarisha mfumo wa ushirikiano wa pamoja.
Siasa za kizalendo
Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier alionya kuhusu siasa za kizalendo , na kutoa wito wa ushirikiano zaidi kimataifa.
"Nafikiri kumekuja wakati ambao utaratibu wa kimataifa umekabiliwa na mbinyo. wanaopendelea ushirikiano wa pamoja na wanapendelea utaratibu huu kuendelea na kuulinda. Ni muhimu kuangalia matumaini hayo na kufanyakazi kwa pamoja katika baraza la Usalama la Umoja wa mataifa."
Dunia haitakuwa na amani kwa mtazamo wa kila mmoja dhidi ya kila mwingine, lakini kwa kutumia ushirikiano zaidi, amesema Steinmeier. Kwa bahati mbaya, si kila mmoja analiangalia suala hilo kwa njia hiyo, ameongeza, bila ya kumtaja rais wa marekani Donald Trump ama kiongozi mwingine wa serikali.
Akiongozana na ujumbe wa ngazi ya juu wa viongozi wa makampuni, Steinmeier, ambaye ziara yake imelenga katika kuimarisha mahusiano baina ya mataifa hayo mawili, alikutana mjini Johannesburg na wawakilishi wa sekta ya biashara na vyama vya kijamii.
Mwandishi: Kroll, Katharina / ZR / Sekione Kitojo
Mhariri: Idd Ssessanga