Steinmeier aapishwa kuwa rais mpya wa Ujerumani
22 Machi 2017Rais mpya wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier katika hotuba yake ya kwanza baada ya kuapishwa alizungumzia juu ya mgogoro unaoendelea baina ya Ujerumani na Uturuki ambapo amemtaka rais wa Uturuki RecepTayyip Erdogan apunguze mvutano huo baina ya nchi hizi mbili. Uturuki imo katika mgogoro na baadhi ya nchi za Ulaya kutokana na wawakilishi wa nchi hiyo kunyimwa ruhusa ya kufanya kampeni kwa ajili ya kura ya maoni itakayofanyika tarehe 16 mwezi April inayolenga kumuongezea rais Erdogan nguvu zaidi. Rais wa Uturuki nchi ambayo ni mwanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO amekuwa akitoa maneno makali kama kuilaumu Ujerumani kwa kutumia mbinu za Kinazi katika kuwazuia mawaziri wa Uturuki kufanya mikutano ya kampeni nchini humu.
Vyama vikuu vya Ujerumani pamoja na kansela Angela Merkel ambaye pia anakiongoza chama cha Christian Demokratic Union (CDU) vilimpendekeza mwanadiplomasia huyo wa zamani katika nafasi hiyo ya urais. Kansela Merkel alisema Steinmeier atakuwa rais bora akitilia maanani kwamba kiongozi huyo anachukua madaraka wakati ambapo nchi inakabiliwa na matatizo mbalimbali.
Watu wengi hapa nchini wanamuona rais mpya Frank Walter Steinmeier mwenye umri wa miaka 61 kuwa sura ya diplomasia ya Ujerumani. Bwana Steinmeier alianza safari yake kama mshauri wa maswala ya sheria katika jimbo la Lower Saxony mnamo mwaka 1991 na baada ya hapo aliendelea kuhudumu katika nyadhfa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa makamu wa kansela na pia mkuu wa shughuli za ofisi ya kansela wa zamani Gerhard Schroeder mnamo mwaka 1999. Mwaka 2005 aliteuliwa kuwa waziri wa mambo ya nje katika serikali ya muungano wa vyama vya Christian Demokratik (CDU) na Social Demokratik (SPD).
Miaka minne baadae alishindwa kwenye kinyang'anyiro cha Ukansela pale alipopambana na kansela Angela Merkel na hapo akawa kiongozi wa upinzani bungeni wa chama chake cha SPD. mwaka 2013 Steimmeier airejea tena katika wadhfa wa waziri wa mambo ya nje katika serikali ya muungano wa vyama inayoongozwa na kansela Angela Merkel.
Rais mpya wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier mtoto wa seremala alisomea uanasheria na maswala ya siasa katika chuo kikuu cha Giessen. Amemwoa jaji Elke Buedenbender na wana mtoto mmoja wa kike. Steinmeier pia atakumbukwa kwa kujitoa katika siasa kwa muda mnamo mwaka 2010 ili kumtolea figo mkewe wakati alipokuwa mgonjwa.
Mwandishi Zainab Aziz/DPAE/AFPE/DW
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman