1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Starmer kuunda 'jeshi la dharura' kukabiliana na vurugu

5 Agosti 2024

Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amesema serikali yake itaunda “jeshi la dharura” linachojumuisha polisi maalum ili kukabiliana na ghasia na matukio ya vurugu yanayoshuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini humo.

https://p.dw.com/p/4j8GK
Uingereza Keir Starmer
Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer.Picha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Kiongozi huyo amesema pia mfumo wa haki utaimarishwa ili kushughulikia kesi za watu wanaokamatwa kufuatia matukio ya vurugu yaliyoitikisa Uingereza hivi karibuni.

Soma zaidi: Vurugu Uingereza: Waziri Mkuu awaonya wavunja sheria

Mapema leo, waziri mkuu huyo aliitisha mkutano wa dharura baada ya kutokea machafuko yaliyochochewa na wanaharakati wa siasa kali za mrengo wa kulia kusambaza habari za uongo kwamba Muislamu mwenye itikadi kali za kidini aliyewasili Uingereza hivi karibuni, ndiye aliyehusika na mauaji ya wasichana watatu mjini Southport, kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Starmer amesema hawatavumilia mashambulizi dhidi ya misikiti na jamii ya Waislamu na kwamba mkono wa sheria utawaandama wote waliohusika na machafuko hayo.