Staffan de Mistura ajaribu kuyafufua mazungumzo ya Syria
16 Februari 2016Msemaji huyo wa Umoja wa Mataifa Ahmad Fawzi amesema, Staffan de Mistura anatarajiwa kukutana kwa mara ya pili na Walid al-Moualem baadaye leo mjini Damascus kujadili kuanzishwa tena mazungumzo ya amani yanayotarajiwa kufanyika tarehe 25 mwezi huu wa Februari, baada ya duru ya kwanza ya mazungumzo kuahirishwa wiki iliyopita.
Katika taarifa fupi aliyoitowa kwa waandishi habari baada ya mkutano wao wa kwanza, de Mistura aliweka wazi yale waliyoyazungumza pamoja na Waziri Moualem.
"Tumekuwa tukizungumzia masuala ya upatikanaji wa misaada ya kibinaadamu kwa maeneo yote yaliyozingirwa sio tu na serikali lakini pia na upinzani na ISIL," alisema de Mistura.
Akizungumza na waandishi habari mjini Geneva, msemaji wa Umoja wa Mataifa Ahmad Fawzi amesema kwa wakati huu kunashuhudiwa uharibifu mkubwa Syria, usiyoweza kuangaliwa bila juhudi zozote kufanyika.
Fawzi ameongeza kuwa sababu zilizofanya mazungumzo kuahirishwa ni kwamba miji kadhaa bado ilikuwa inashambuliwa na raia walikuwa wanaendelea kukabiliwa na njaa.
Hata hivyo viongozi wa mataifa yaliyo na nguvu duniani walikubaliana siku ya ijumaa katika mkutano wa usalama uliyofanyika mjini Munich Ujerumani, kukomesha uhasama nchini Syria ili misaada ya kiutu iweze kutolewa, lakini mpango huo haujaanza kutekelezwa hadi mwishoni mwa wiki hii na haukutiwa saini na pande zinazohasimiana.
Uturuki yaishutumu Urusi kutekeleza uhalifu wa kivita
Wakati huo huo Uturuki hapo jana iliishutumu Urusi kutekeleza uhalifu wa kivita, baada ya mashambulizi ya maroketi Kaskazini mwa Syria, kusababisha vifo vya takriban watu 50, huku ikitoa onyo kwa wapiganaji wa kikurdi kwamba watapambana na majibu makali kutoka iwapo watajaribu kuudhibiti mji uliyoko karibu na mpaka wake.
Kwa upande wake msemaji wa Umoja wa Mataifa wa haki za binaadamu Rupert Colville amelaani mashambulizi ya angani yaliyofanywa hapo jana katika hospitali na shule mjini Idlib na Aleppo.
Kwengineko rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk amesema mashambulizi ya angani yanyofanywa na Urusi nchini Syria huenda yakatatiza mpango wa kusimamishwa mapigano katika nchi hiyo iliyo katika mapigano kwa miaka mitano sasa.
Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu