SPD yawachagua Norbert Walter-Borjans na Saskia Esken
1 Desemba 2019Hali hiyo inazusha maswali mengi kuhusiana na hatima ya serikali ya Ujerumani. Chama cha SPD kimesema mfuasi wa siasa za mrengo wa kushoto Norbert Walter-Borjans na Saskia Esken, ambao waligombea kwa tikiti ya pamoja, walishinda asilimia 53.06 ya kura zilizopigwa na wanachama. Wanataka kujadili upya muungano unaounda serikali kulenga zaidi kuhusu haki ya kijamii, uwekezaji na sera za mazingira.
Hata hivyo , uwezekano wa uchaguzi wa haraka ama serikali yenye wingi mdogo bungeni umeongezeka wakati wahafidhina wanaoongozwa na Merkel huenda wakakataa kutoa ushirikiano licha ya kuwa watapendelea kubakia mabadarakani.
Chama cha SPD , chama kikongwe kabisa nchini Ujerumani, kimeingia katika vurumai baada ya kupata matokeo mabaya katika chaguzi za majimbo na uchaguzi wa bunge la Ulaya pamoja na mbio za miezi sita kuwania uongozi ambazo zimesababisha chama hicho kuporomoka katika maoni ya wapiga kura. Wanachama wengi katika uongozi wa chama hicho wanona kuwa kuokoka kwao ni kujitoa tu kutoka katika serikali na kujenga upinzani.
Pigo kwa Scholz
Wafuasi hao wawili wa siasa za mrengo wa kushoto waliwashinda waziri wa fedha Olaf Scholz na Klara Geywitz, ambao walisema watawaunga mkono mahasimu wao baada ya ushindi wa asilimia 45.33 ya kura.
Matokeo hayo ni pigo kubwa kwa Scholz, mgombea ambae ni maarufu zaidi. Vyombo vya habari vya Funke vimeripoti kuwa hakusudii kubakia kuwa waziri wa fedha.
Baada ya ushindi wao wa kushitukiza, Walter-Borjans, waziri wa fedha wa zamani katika jimbo lenye wakaazi wengi nchini Ujeruani la North Rhine-Westphalia na Esken, mbunge katika bunge la Ujerumani , Bundestag, wameahidi kukileta chama hicho pamoja na kujenga umoja miongoni mwa wanachama na viongozi.
Walter-Borjans, ambaye amepata umaarufu akifahamika kama "Robin Hood" kwa kupambana na wale wanaokwepa kulipa kodi katika benki za Uswisi, amesisitiza kuwa chama cha SPD hakitautupilia mbali muungano wa serikali mara moja.
"Tumesema mara nyngi hii sio juu ya iwapo tunaondoka mara moja ama kubakia kwa kipindi fulani," aliiambia televisheni ya Phoenix, na kuongeza kuwa analenga kuangalia sera gani zinaweza kutekelezwa pamoja na chama cha Merkel na zipi haziwezekani.
Viongozi hao wawili wamesisitiza kwamba wanataka wahafidhina kukubaliana na kiwango cha juu cha mshahara wa kima cha chini na uwekezaji zaidi katika miundo mbinu pamoja na ulinzi wa mazingira, iwapo itahitajika hata kwa kuwa na deni jipya.
Katibu mkuu wa chama cha Christian Democrats CDU amesema chama chake kinataka kufanyakazi pamoja na uongozi mpya wa SPD na kwamba vyama hivyo tayari vina msingi wa pamoja wa kufanyia kazi.