SPD yapata ushindi wa jimbo la Hamburg
24 Februari 2020Wakati huo huo inaelekea wapiga kura wamekiadhibu chama cha kihafidhina cha kansela Angela Merkel na kupata matokeo mabaya kabisa jimboni Hamburg jana.
Chama cha walinzi wa mazingira cha Kijani, chama ambacho kimekuwa katika serikali ya muungano pamoja na SPD kwa miaka mitano iliyopita katika jimbo hilo, kimechukua nafasi ya pili kikipata asilimia 24.2, na kuongeza mara dufu kura ilizopata katika uchaguzi uliopita mwaka 2015. Matokeo hayo yana maana serikali ya muungano kati ya vyama hivyo inaendelea.
Chama cha kansela Angela Merkel cha Christian Democratic Union, CDU kimepata matokeo mabaya kabisa ya bunge la majimbo kwa zaidi ya miaka 70, kikipata asilimia 11.2 tu ya kura.
Chama cha siasa kali za mrengo wa kushoto cha Die Linke , kimefanikiwa tu kuongeza idadi ya asilimia ya kura zake kutoka asilimia 8.5 hadi asilimia 9.1.
Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Alternative for Germany , chama mbadala kwa Ujerumani ,AfD kimepata asilimia 5 na kile kinachopendelea wafanyabiashara cha Free Democrats FDP kimepata asilimia 5.3, na kujihakikishia kupata uwakilishi bungeni.
Chama cha AfD
Katika uchaguzi wa mwaka 2015 chama cha AfD kilipata asilimia 6.1 ya kura na kilishuhudiwa kikiingia katika bunge kwa mara ya kwanza katika upande wa magharibi nchini Ujerumani, lakini kabla ya hapo kilikuwa kina uwakilishi katika majimbo ambayo yalikuwa ya iliyokuwa Ujerumani mashariki ya zamani. Chama hicho sasa kinauwakilishi katika majimbo yote 16 ya Ujerumani.
Chama cha kihafidhina cha Christian Democratic Union , CDU kimepata kipigo baada ya kiongozi wa chama hicho na mteule wa kansela Merkel Annegret Kramp-Karrenbauer kusema atajiuzulu, na kufungua mbio za kuwania kurithi kiti cha kansela na kukitumbukiza chama hicho katika mtafaruku.
Hii ni kutokana na hali iliyojitokeza katika uchaguzi wa jimbo la Thuringia, ambapo chama hicho kilijaribu kukaribiana na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD katika uchaguzi wa jimbo hilo la mashariki na hali hiyo imekitumbukiza chama cha hicho katika mpambano wa kuwania madaraka. Wanachama waandamizi wa chama hicho wanakutana leo Jumatatu kuamua kuhusu mpango wa uongozi mpya wa chama hicho , baada ya kushindwa vibaya katika uchaguzi wa Hamburg hali inayozidi kuleta dharura ya kusaka haraka uongozi wa juu wa chama hicho.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / dpae
Mhariri: Yusuf Saumu