SPD wasaka uungaji mkono wa makubaliano pamoja na CDU/CSU
16 Januari 2018Tunaanza na kishindo kinachowasumbua wana SPD katika dhamiri yao ya kutaka kuundwa serikali ya muungano pamoja na vyama ndugu vya kihafidhina CDU/CSU. Wengi miongoni mwa viongozi wa chama hicho kikongwe zaidi miongoni mwa vyama vya kisiasa nchini Ujerumani, hawaungi mkono makubaliano yaliyofikiwa ijumaa iliyopita baada ya siku sita za kutathmini uwezekano wa kuunda serikali hiyo ya muungano wa vyama vikuu, maarufu kama GroKo. Gazeti linalosomwa na wengi na kuelemea zaidi mrengo wa kulia,"Bild" linajiuliza viongozi wa SPD wana maana gani kama hawana nguvu za kuamua? Gazeti linaendelea kuandika: "Bild linakumbusha mkutano mkuu wa dharura utakaoitishwa Jumapili inayokuja na ambao ndio utakaoamua kama mazungumzo ya kuunda serikali pamoja na vyama ndugu vya CDU/CSU yaanze. Baadae wanachama 440.000 wa SPD watatakiwa kupiga kura kwa njia ya barua kama serikali iundwe nchini Ujerumani. Pekee kuwauliza wanachama maoni yao linakiuka umuhimu wa kuwa mwanachama. Kinachotajwa kuwa demokrasia ya mashinani si chochote chengine isipokuwa patashika inayosababishwa na udhaifu na hali ya kutojiamini. Kauli mbio hapo: amueni nyie, ili tusije tukaambiwa ni makosa yetu. Udhaifu sawa na huo unajitokeza pia upande wa chama cha CDU cha Angela Merkel na CSU cha Horst Seehofer vinavyochangia katika kasheshe hiyo. Hata FDP walitaka kuwauliza maoni yao wanachama wao pindi mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano wa Jamaica yangefanikiwa. Hapo wanachama 64.000 wangewaamulia raia milioni 80 wa Ujerumani. Kizungumkuti chetu sote hapo ni kwamba maamuzi yanayopitishwa katika hali ya udhaifu ni nadra kuleta mafanikio."
Die Linke yataka kuyaleta pamoja makundi ya mrengo wa kushoto
Chama cha siasa kali za mrengo wa kushoto die Linke kimepania kuyaleta pamoja makundi yote ya mrengo wa kushoto humu nchini na kubuni vuguvugu la mrengo wa kushoto. Fikra hiyo imezushwa na mwenyekiti wa chama hicho Sarah Wagenknecht. Fikra hiyo inapingwa lakini miongoni mwa viongozi wa chama hicho.Gazeti la Hannoversche Allgemeine linaandika: "Mrengo wa kushoto nchini Ujerumani haujafanikiwa hadi wakati huu kupata jibu la kishindo kinachosababishwa na kuzidi kupata nguvu vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia vinavyoifuja mandhari ya kisiasa barani Ulaya na kumfungulia milango ya kuingia ikulu ya Marekani White House, Donald Trump. Kinachotakiwa ni uwiano madhubuti wa raslimali na haki katika karne ya 21. Mada hiyo ina umuhimu mkubwa kuliko kuachiliwa iingie katika mradi wa kibinafsi wa mtu na mumewe, Oscar Lafontaine na Wagenknecht."
Matumizi ya nguvu ni ya kulaaniwa
Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu matumizi ya nguvu dhidi ya polisi. Gazeti la Passauer Neue Presse linaandika: "Na awe, muafghani, muiran au mjerumani, matumizi ya nguvu dhidi ya polisi au mtu yeyote mwengine ni kitendo cha kulaaniwa. Na aliyosema waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la kusini la Bavaria Joachim Herrmann kwamba wakimbizi wanabidi kufuata sheria za humu nchini, yanastahiki kuungwa mkono. Kwasababu anaeomba kinga ya ukimbizi humu nchini anajiharibia mwenyewe anapokutikana na hatia ya matumizi ya nguvu.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Iddi Ssessanga