Siku ya kimataifa ya kutokomeza manyanyaso kwa wazee
15 Juni 2023Makaazi ya wazee ya Mapeera Kateyamba mtaa wa Nalukolongo mjini Kampala hushughulikiwa na watawa wa Kikatoliki wa jumuiya ya msamaria mwema.
Kuwepo kwa makao hayo ni kielelezo kuwa kuna wazee wasiobahatika katika jamii na wanapotelekezwa na jamaa zao hapa ndipo wanakokimbilia. Miongoni mwa wazee hao ni wale kutoka mataifa jirani waliojikuta mashakani baada ya kutengwa au kutengana na jamaa zao.Oktoba mosi: Siku ya Kimataifa ya wazee duniani
Kinyume na utamaduni na maadili ya Kiafrika, idadi ya wazee wanaojikuta katika hali hii inaongezeka. Katika makaazi haya pekee kuna wazee 75 wa kiume na kike.
Hali halisi ni kwamba wazee wanazidi kunyanyaswa na kudhulumiwa kuanzia ngazi ya familia ambapo mienendo ya kuwatelekeza inashuhudiwa. Miongoni mwa manyanyaso na dhuluma dhidi ya wazee ni kutukanwa, kupigwa na kuteswa kimwili ikiwemo kubakwa kwa upande wa wanawake. Aidha, baadhi hudhulumiwa mali zao kama vile ardhi na hata pesa zao.
Katika baadhi ya jamii, wazee hushambuliwa kwa madai kwamba wao ni wachawi. Haya na mengine mengi huwatia katika hali ya upweke na unyanyapaa na kwa hiyo kuteseka kimawazo. Hiki ndicho chanzo cha baadhi yao kuugua ugonjwa wa akili.
Huku idadi ya wazee ikiongezeka kwa kasi kote duniani kutokana na kuimarika kwa huduma za afya, wadau wanakumbusha kuwa kadri wazee wanavyozidi kunyanyaswa na kutelekezwa, haki zao za msingi za binadamu zinakiukwa.