1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya Kimataifa ya kukomesha uhalifu dhidi ya wanahabari

2 Novemba 2021

Tarehe 2 Novemba dunia huadhimisha siku ya kukomesha mienendo ya kutoshughulikia uhalifu unaofanywa dhidi ya wanahabari, ikiwa ni pamoja na mauaji, hujuma na pia vifaa vyao kuharibiwa.

https://p.dw.com/p/42Sse
Uganda Journalist David Musisi Kalyankolo
Picha: DW/Julius Mugambwa

Kulingana na takwimu zilizokusanywa mwaka huu wa 2021 na mashirika kadhaa yanayopigania haki za wanahabari duniani, kiwango cha kutowadhibu wale wanaowanyanyasa wanahabari kingali cha juu kwa asli mia 87 sawa na miaka iliyotangulia. Hii ina maana hali hii haijaboreka kwani kwa mfano kati ya wanahabari 139 waliouawa kati ya mwaka 2011 na 2020, asli mia 41 kati yao walipokea vitisho kabla ya kuuawa.

Kinacholeta kero zaidi ni kwamba wengi wanahabari waliouawa au kuhujumiwa, wao hufanyiwa uhalifu huo ndani ya nchi zao. Ni kwa ajili hii ndipo mwito unatolewa kuwa chanzo cha kufanikisha uhuru wa kujieleza wa wanahabari ni kulinda haki za wale wanaotendewa maovu kupitia michakato ya kisheria lakini pia kuwahusisha wanajamii kufahamu umuhimu wa wanahabari.

Gawaya Tegule ni mwanahabari na pia mwanaharakati wa haki za binadamu, amesema shambulizi dhidi ya wanahabari ni shambulizi dhidi ya watu na haki yao ya kupata habari au taarifa wanazohitaji

Soma zaidi: Polisi Tanzania yashutumiwa kwa kuhangaisha wanahabari

Katika muda wa miaka 14 tangu mwaka 2006 hadi sasa, zaidi ya wanahabari 1,200 duniani wameuwa kwa kuchapisha habari na kutoa taarifa kwa umma. Huku mauaji yakiwa ndiyo kilele cha uhalifu dhidi ya wanahabari, hatua za taasisi za serikali kudhibiti shughuli za wanahabari huonekana kuwa chanzo cha kuwatishia kuendesha kazi zao.

Waandishi habari Uganda wadai huenda kuna njama za kuwakandamiza zaidi

Uganda | Journalisten am Uganda Media Center
Baadhi ya waandishi habari Uganda Picha: Lubega Emmanuel/DW

Mabishano kuhusu kuwasajili wanahabari nchini Uganda hivi karibuni ni mojawapo ya vielelezo kuwa wanahabari wanadhani watakandamizwa. Baadhi ya wanahabari walinukuliwa hivi pale waziri wa habari Uganda Chris  Baryomunsi aliposisitiza kuwa lazima wasajiliwe licha ya mahakama kutoa agizo shughuli hiyo isimamishwe.

" Kila wanahabari wanapokabiliana na shida kwa mfano wanapokabiiana na vyombo vya usalama au kupigwa hatuoni serikali ikisema kitu" walisema baadhi ya wanahabari

soma zaidi: Onyo la Baraza la Waandishi wa Habari kwa wanasiasa nchini Kenya

Kwa upande mwingine, wanahabari wanakosolewa kwa kuendeleza tabia ya kesi zao kutoshughulikiwa ipasavyo pale wanapoamua kuziondoa kwenye mchakato wa kisheria au kukataa kuwashtaki na kuwatambulisha wale wanaowanyanyasa.

Wakati dunia ikiadhimisha siku hii, shirika la Umoja Mataifa UNESCO linasisitiza kuwa vyombo vya kisheria ni wadau wakuu katika kukomesha uhalifu dhidi ya wanahabari kutoadhibiwa. Aidha, mwito unatolewa kwa wanajamii kuwaondolea unyanyapaa na pia kuwaliwaza wanahabari wanaonyanyaswa.

Mwandishi: Lubega Emmanuel DW Kampala.