Shirika la Ushirikiano la Shanghai laikaribisha rasmi Iran
4 Julai 2023China na Urusi katika miaka ya hivi karibuni zimezidisha ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia huku ushirika wao wa kimkakati ukionekana kuimarika zaidi tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mnamo mwaka jana.
Katika mkutano huo wa kilele wa Shirika la ushirikiano wa Shanghai SCO uliofanyika India kwa njia ya video, Rais Xi Jinping wa China "amehimiza juhudi za kulinda amani ya kikanda na kuhakikisha usalama wa pamoja," akizitaka nchi wanachama wa SCO "kuimarisha mshikamano wao". Aidha Xi ameonya dhidi ya kile alichokitaja kuwa "mapinduzi dhidi ya serikali" na "zama mpya za vita baridi".
"China iko tayari kufanya kazi na pande zote ili kutekeleza mpango wa kimataifa wa maendeleo, kuweka mwelekeo sahihi wa utandawazi wa uchumi, sera ya kulinda viwanda, vikwazo vya upande mmoja na kuzidisha usalama wa taifa na kukataa hatua za kuweka vikwazo. Tunapaswa kufanya ushirikiano wenye ushindi mkubwa zaidi na kuhakikisha kuwa faida zaidi za maendeleo zitashirikiwa kwa haki na watu kote ulimwenguni," alisema Xi.
Akizungumza kwa njia ya video ikiwa ni mkutano wake wa kwanza wa kilele tangu kulipotokea jaribio la uasi mwezi uliopita wa kundi la mamluki la Wagner, Rais wa Urusi Vladimir Putin amelishukuru shirika la ushirikiano la Shanghai kwa namna walivyomuunga mkono. Amesema Urusi "inapinga kwa ujasiri na itaendelea kupinga shinikizo kutoka nje, vikwazo na uchochezi". Amelihakikishia jukwaa hilo kwamba "Warusi wamekuwa wamoja" kuliko ilivyokuwa awali.Viongozi wa kundi la BRICS watia saini tamko la pamoja
"Hivi sasa kimsingi, vita mamboleo inafanywa dhidi yetu, vikwazo haramu dhidi ya Urusi vinatumika kwa kiwango ambacho hakijawahi kutokea. Ningependa kusisitiza kwamba Urusi inapinga kwa ujasiri na itaendelea kupinga shinikizo la nje, vikwazo na uchochezi. Na katika hali ya sasa, nchi yetu inaendelea kukua kwa kasi," amesema Putin.
Katika mkutano wa kilele wa Shirika la Ushirikiano wa Shangai uliofanyika India, Iran imekaribishwa kujiunga rasmi kuwa mwanachama wa tisa wa jukwaa hilo, ambapo jitihada zake za kusaka ushirikiano wa kidiplomasia na washirika wake wa karibu zinaonekana kushika kasi, lengo likiwa ni kupunguza hali ya kutengwa na kuimarisha uchumi wake. Rais wa Iran Ebrahim Raisi amesema uanachama wa Tehran utasaidia katika "usalama wa pamoja, kupanua uhusiano, mawasiliano sambamba na kuimarisha umoja."
Sambamba na mwenyeji wa mkutano huo India, nchi zingine wanachama ni China, Urusi, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Pakistan, Tajikistan, Uzbekistan na Iran.
Vyanzo: afp/reuters