Shinikizo laongezeka dhidi ya India ilaani uvamizi wa Urusi
2 Machi 2022India bado haijaikosoa hadharani Urusi ambayo kwa muda mrefu inaiuzia silaha na badala yake imezihimza Urusi na Ukraine kusitisha mapigano hatua ambayo imesababisha mafadhaiko miongoni mwa washirika wake wengine ikiwa ni pamoja na Marekani.
Maelfu ya raia wa India bado wamekwama nchini Ukraine na kusababisha miito kwa serikali kuongeza shinikizo dhidi ya Urusi kusaidia katika juhudi za uokozi.
Katika ujumbe alioandika katika mtandao wa twitter, P. Chidambaram, mbunge wa chama pinzani cha Congress, amesema kuwa serikali ya India inapaswa kukoma kupima maneno yake na kutoa wito thabiti kwa Urusi kusitisha mara moja kushambulia kwa mabomu miji mikubwa nchini Ukraine.
India yakosa kushiriki katika kura dhidi ya Urusi
India haikushiriki katika kura ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulaani uvamizi huo wiki iliyopita, ingawa katika siku za hivi karibuni imekuwa ikitoa kauli zisizobainika kwa uwazi.
Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya India iliyotolewa Jumanne jioni, imesema kuwa waziri mkuu Narendra Modi alisisitiza kuhusu umuhimu wa kuheshimu uhuru na uadilifu wa mipaka ya mataifa wakati wa mazungumzo yaliofanyika kwa njia ya simu na rais wa Poland Andrzej Duda.
Taarifa hiyo imeongeza kusema kuwa India imechukua msimamo mkali kwa faragha na Rais wa Urusi Vladimir Putin.
Kwa muda mrefu, Urusi imekuwa ikiiunga mkono India kimataifa katika masuala muhimu yanayolijumuisha eneo la Kashmir lililozua mvutano kati ya India, Pakistan na China pamoja na kuimarisha kwa kiasi kikubwa uwezo wa jeshi lake.
India imekuwa ikijaribu kupunguza utegemezi wa silaha za Urusi
Kwa muda mrefu, India imejaribu kupunguza utegemezi wake wa silaha zinazotengenezwa na Urusi huku ikiweka uhusiano wao karibu kuizuia Urusi kushirikiana zaidi na taifa pinzani lenye nguvu, China.
Harsh Pant, mchambuzi wa masuala ya ulinzi na siasa za kijiografia katika taasisi ya utafiti wa uangalizi yenye makao yake mjini New Delhi, amesema kuwa India haijaridhishwa na hatua iliyochukuliwa na Urusi lakini inakabiliwa na uzito wa kuilaani hadharani.
Pant amesema kuwa asilimia 60 ya vifaa vya kijeshi vya India bado vimetengenezwa na Urusi na uhusiano na Urusi ni muhimu kudumisha usambazaji wa vifaa na chanzo cha kupata vipuri vya vifaa hivyo.