Sheria ya kuvaa hijab kupitiwa upya nchini Iran
29 Aprili 2024Kulingana na taarifa iliyotolewa na shirika la Tasnim, iwapo muswaada huo wa sheria utaidhinishwa, adhabu kali zinaweza kutolewa kwa wanaokiuka kanuni za mavazi ya taifa hilo la Kiislam, pamoja na kuwataka wanawake kufunika nywele zao hadharani.
Mjadala mkali kuhusu sheria inayopendekezwa umekuwa ukiendelea nchini Iran tangu mwaka jana, huku baadhi ya wabunge wenye misimamo mikali wakisisitiza kwamba adhabu zilizopo ni nyepesi huku wanasiasa wa wastani wakipinga vikali adhabu hizo.
Pendekezo hilo linatoa adhabu kali, ikiwamo kifungo cha hadi miaka 15 jela na kutozwa faini ambayo ni sawa na zaidi ya dola 5,000.
Wanawake wa kigeni wanaweza kufukuzwa nchini humo, na watu mashuhuri kuadhibiwa vikali, rasimu hiyo pia itaweka marufuku ya kitaaluma ya hadi miaka 15.