Shehena ya kwanza ya misaada kuelekea Gaza yapakuliwa
16 Machi 2024Kupitia taarifa, shirika hilo limeeleza kuwa shehena hiyo ya misaada yenye takriban tani 200 za chakula imeshushwa na iko tayari kusambazwa.
"World Central Kitchen" imelazimika kujenga gati kusini magharibi mwa Gaza ili kusaidia kupakua na kuisambaza misaada hiyo.
Shirika hilo la hisani la Marekani linaanda safari ya mashua ya pili yenye msaada mwengine wa karibu tani 240 za chakula kutokea Cyprus, kituo cha kwanza cha njia mpya ya bahari ya kupeleka misaada Mediterania ya mashariki.
Soma pia: Meli ya misaada kutoka Cyprus taratibu yakaribia Gaza
Misaada hiyo inajumuisha vyakula vya mkebe ikiwa ni pamoja na bidhaa nyengine kama vile maharagwe, karoti, samaki aina ya jodari, mbaazi, mahindi, mchele, mafuta na chumvi.
Jeshi la Israel limethibitisha kuwa, meli ya kwanza inayoendeshwa na shirika la misaada la Uhispania la Open Arms, pia imewasili na kwamba wanajeshi wake wametumwa katika bandari ili kushika doria na kufanya ukaguzi.