1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulizi la Israel laua watano Ukingo wa Magharibi

14 Agosti 2024

Wapalestina watano wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel na kwenye msako uliofanyika kaskazini mwa eneo linalokaliwa la Ukingo wa Magharibi.

https://p.dw.com/p/4jRdz
Wanajeshi wa Israel wakiwa katika msako karibu na Tubas, Ukingo wa Magharibi
Wanajeshi wa Israel wakiwa katika msako karibu na Tubas, Ukingo wa MagharibiPicha: JAAFAR ASHTIYEH/AFP

Jeshi la Israel limesema limefanya mashambulizi ya anga dhidi ya magaidi wenye silaha kwenye mji wa Tammun, mapema Jumatano umbali wa kilomita tano kutoka Tubas. Gavana wa Tubas, Ahmad Saad amesema Wapalestina watano wameuawa Tammun na mmoja Tubas.

Miili ya waliouawa inashikiliwa na Israel

Kulingana na Saad, wanajeshi wa Israel wanaishikilia miili ya mashahidi hao watano. Shirika rasmi la habari la Kipalestina, Wafa, limeripoti kuwa jeshi liliingia Tubas mapema Jumatano alfajiri na kumuuwa kwa kumpiga risasi kijana mmoja aliyekuwa amejificha nyumbani kwake.

Jeshi la Israel limethibitisha kuwa limeanzisha operesheni ya ''kupambana na ugaidi'' kwenye mji huo, ambapo ilisababisha kifo cha gaidi mmoja na kuwashambulia wengine wakati wa majibizano ya risasi. Kulingana na jeshi hilo, wanajeshi wake wamewakamata washukiwa wanaosakwa na kukamata silaha.

Rais wa Marekani, Joe Biden
Rais wa Marekani, Joe BidenPicha: Eric Gay/AP Photo/picture alliance

Huku hayo yakijiri Rais wa Marekani Joe Biden amesema makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza yataizuia Iran kuishambulia Israel kulipiza kisasi kwa mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas, Ismail Haniyeh aliyeuawa mjini Tehran. Akizungumza na waandishi habari siku ya Jumatatu, Biden amesema hali inazidi kuwa ngumu, lakini hawatokata tamaa.

Biden na dhamira ya kuleta suluhisho la amani

''Tutaona kile Iran itakifanya, na tutaona kitakachotokea iwapo kutakuwa na shambulizi lolote. Lakini sikati tamaa. Hayo ni matarajia yangu, lakini tutaona,'' amefafanua Biden. Rais huyo wa Marekani amesisitiza umuhimu na dhamira yake ya kuleta suluhisho la kusimamisha mapigano huko Gaza.

Wakati huo huo, mjumbe maalum wa Marekani Amos Hochstein, anatarajiwa kuwasili Jumatano mjini Beirut, katika ziara muhimu yenye lengo la kupunguza mvutano kati ya Israel na kundi la Hezbollah la Lebanon. Duru za serikali ya Lebanon zimeeleza kuwa akiwa Beirut, Hochstein anatarajiwa kukutana na Spika wa Bunge, Nabih Berri, mshirika wa karibu wa Hezbollah, pamoja na Waziri Mkuu Najib Mikati.

Mjumbe maalum wa Marekani Amos Hochstein (kushoto) akiwa na Spika wa Bunge la Lebanon, Nabih Berri
Mjumbe maalum wa Marekani Amos Hochstein (kushoto) akiwa na Spika wa Bunge la Lebanon, Nabih BerriPicha: Bilal Hussein/AP Photo/picture alliance

Mjumbe huyo wa Marekani amekuwa akijaribu kutafuta suluhisho la kidiplomasia kati ya Israel na Hamas kwa miezi kadhaa sasa, ingawa ziara zake za mara kwa mara katika ukanda huo, bado hazijaleta utulivu katika mpaka wa kusini mwa Lebanon. Kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran limeapa kulipiza kisasi baada ya Israel kumuua kamanda wake wa kijeshi Fuad Shukr mjini Beirut, wiki mbili zilizopita.

Umoja wa Mataifa: Kuna haja ya kusitisha vita

Ama kwa upande mwingine, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa wito wa hatua zaidi kuchukuliwa ili kuepusha kuzuka kwa mgogoro.

Akizungumza katika mkutano wa dharura wa baraza hilo, Rosemary Di Carlo, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kisiasa na Ujenzi wa Amani, amesema shambulizi la Israel katika shule ya al-Tabeen huko Gaza, limechochea kufanyika kwa mkutano huo, na linaonyesha kwa mara nyingine tena haja kubwa ya kufikia makubaliano ya kusitisha vita, kuachiliwa kwa mateka na kuongeza misaada ya kiutu huko Gaza.

Israel yazidisha mashambulizi katika ukanda wa Gaza

(AFP, DPA, AP, Reuters)