Ujerumani yaidhinisha vifaru vya Leopard kwa Ukraine
25 Januari 2023Matangazo
Msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Hebe-streit amesema hatua ya kwanza itakayochukuliwa ni kutoa vifaru hivyo 14 kutoka katika hifadhi yake ya kijeshi.
Akiizungumzia hoja hiyo hii leo bungeni Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema kando na kutoa vifaru hivyo Ujerumani itatoa mafunzo pia kwa wanajeshi wa Ukraine.
Scholz amesema nchi yake mara zote itakuwa mstari wa mbele linapokuja suala la kuiunga mkono Ukraine. Poland na Uingereza, ambazo zimeahidi mizinga 14 kila moja, zimekaribisha uamuzi huo.
Uholanzi, Finland na Uhispania zimesema pia zilikuwa tayari kupeleka vifaru hivyo. Ukraine imeishukuru Ujerumani kwa hatua hiyo, huku Urusi ikilaani na kusema Ujerumani imetelekeza wajibu wake kwa Moscow.