1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Uingereza yaahirisha bunge lake kwa wiki tano.

10 Septemba 2019

Serikali ya Uingereza imeahirisha rasmi vikao vyake vya bunge hii leo na kuwapa wabunge likizo ya wiki tano huku mzozo wa nchi hiyo kujiondoa katika Umoja wa Ulaya, Brexit ukiendelea.

https://p.dw.com/p/3PK21
UK Brexit | Parlament
Picha: AFP/HO

Bunge limeahirishwa rasmi lakini ni baada ya Spika John Bercow kuelezea kutoridhishwa kwake na kusema wengi wanachukulia suala hili kuwa ''hatua ya uamuzi wa viongozi wakuu''. Kulikuwa na visa kadhaa vya upinzani kupiga kelele kukosoa hatua hii ya kulisitisha bunge wakisema serikali ya Waziri Mkuu Borris Johnson "imekosa aibu."

Wakati wa kikao cha mwisho bungeni, wabunge wamekataa ombi la waziri mkuu huyo la uchaguzi kabla ya nchi hiyo kujiondoa katika Umoja wa Ulaya mwezi ujao. Ni wabunge 293 tu kati ya 650 waliounga mkono pendekezo hilo, hii ikiwa ni idadi ya chini ya thuluthi mbili zinazohitajika za wingi wa kura. Wabunge wa upinzani walipiga kura dhidi ya pendekezo hilo na wengine kutoshiriki kabisa.

Johnson anataka kura ya mapema tarehe 15 mwezi Oktoba hii ikiwa ni wiki mbili kabla ya tarehe 31 Oktoba iliyopangiwa kwa Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya. Lakini vyama ya upinzani vinasema kuwa havitaunga mkono uchaguzi wowote hadi pale Uingereza  itakapotafuta kuongezwa kwa muda wa kujiondoa katika Umoja wa Ulaya kuhakikisha kwamba nchi hiyo haiondoki katika Umoja huo bila mkataba.

Bunge limeiagiza serikali kutafuta makubaliano ya kuongeza muda wa Brexit iwapo hakutakuwa na mkataba kufikia mwisho wa Oktoba, lakini Johnson ameapa kutoongeza muda huo. Bunge linarejelea vikao vyake tarehe 14 Oktoba hii ikiwa ni takriban wiki mbili kabla ya Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya tarehe 31 mwezi Oktoba.

Upande wa upinzani unamlaumu Waziri Mkuu Boris Johnson kwa kujaribu kuwazuia wabunge kuupitia mpango wake wa Brexit.Hii ni mara ya kwanza katika zaidi ya miaka 70 ambapo serikali ya Uingereza imesitisha vikao vya bunge baada ya kukabiliwa na upinzani.