1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Tanzania yaonya kuhusu kutoa taarifa za COVID

Admin.WagnerD5 Machi 2021

Serikali ya Tanzania imetoa onyo kali dhidi ya wale wanaotoa na kusambaza taarifa kuhusiana na magonjwa ya mlipuko ikiwamo janga la maambukizi ya virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/3qFhD
Tansania | Dr. Hassan Abbas
Picha: DW/S. Khamis

Karipio hilo la serikali ya Tanzania linatolewa wakati kukiwa na matamko kadhaa kutoka kwa madhehebu ya kidini yanayotaka uwazi katika kushughulikia janga hilo ambalo linaendelea kuisumbua dunia. 

Msemaji mkuu wa serikali Dkt. Hassan Abbas ameonya kuwa ni kinyume na taratibu kuona mtu akichukua uamuzi wa kutoa taarifa zinazohusiana na majanga kama vile mlipuko wa maambukizi ya virusi vya corona.

Soma Zaidi: Maafisa wa serikali Tanzania wapuuza uvaaji barakoa

Abbas ameeleza kuwa serikali imeweka utaratibu ambao unabainisha wazi ni nani mwenye mamlaka ya kutoa taarifa za namna hiyo. Amefahamisha kuwa serikali imelazimika kujitokeza kubainisha jambo hilo hasa baada ya kuendelea kushuhudia mwenendo mpya aliouita kwa baadhi ya watu kutumia njia mbalimbali kusambaza taarifa ambazo haziko ndani ya mamlaka yao.

Ingawa tangu mwaka uliopita hakuna takwimu zote zilizotolewa na serikali kuhusiana na idadi ya waliokumbwa na janga hilo wala wale waliopoteza maisha, serikali hiyo imeendelea kusisitiza kuwa inaamini iko katika mkondo sahihi katika kukabiliana na ugonjwa huo wa covid 19.

Tansania Dar es Salaam | Grafitty zu Corona
Tangazo linaloonyesha namna ya kujikinga na maambukizi ya corona Picha: Eric Boniphace/DW

Dr Abbas amesema, serikali inaendelea kuchukua tahadhari zote kukabiliana na janga hilo na anasema hadi wakati huu janga hilo ambalo linaendelea kuwa mwiba duniani limedhibitiwa vyakutosha nchini Tanzania.

Pamoja na kwamba, msemaji huyo wa serikali hakuweka bayana ni kina nani ambao wamekuwa wakitoa takwimu na taarifa kuhusiana na maambukizi ya janga hilo, hata hivyo hivi karibuni baadhi ya makanisa yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara kuzungumzia janga hilo.

Lakini kanisa Katoliki ndilo lililokwenda mbali zaidi kwa kuweka mwongozo unaopaswa kufuatwa na waaumini wake wakati wanaposhiriki ibada makanisani na namna watavyoadhimisha sikuu ya Pasaka.

Mbali na hilo, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu, Padre Charles Kitima alielezea jinsi kanisa hilo linavyokumbwa na majonzi baada ya kupoteza makasisi wake 25 katika kipindi cha miezi miwili iliyopita kutokana na matatizo yaliyoambatana na upumuaji.

Hadi sasa ingawa baadhi ya nchi ndani ya Afrika Mashariki zimeanza kupokea chanjo dhidi ya virusi vya corona, Tanzania bado haijafungua milango kuruhusu chanjo hiyo inayotolewa kupitia mpango wa kimataifa wa kusaidia nchi masikini ujulikanao Covax.

Soma Zaidi: Rais Magufuli atoa tahadhari ya uvaaji wa barakoa kutoka nje

Hospitali ya taifa Tanzania yazindua huduma ya kujifukiza

George Njogopa.