1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Haftar alitangaza kusitisha mapigano mnamo Juma tano

Ibrahim Swaibu
1 Mei 2020

Wito wa Haftar ulijiiri baada ya serikali ya GNA kuvifurusha vikosi vya mbabe huyo wa kivita  kutoka katika ngome zake mbili zilioko magharibi mwa Tripoli

https://p.dw.com/p/3bf8M
Libyen General Khalifa Haftar
Picha: picture-alliance/dpa/T. Stavrakis

Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNA) inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa imekataa hatua ya upande wa mbabe wa kivita Khalifa Haftar ya usitishwaji wa operesheni za kijeshi uliotangazwa Jumatano.

Kupitia kwenye taarifa yake iliotolewa Alhamsi, serikali hiyo ya Tripoli ilisema haina imani katika Haftar na kumtuhumu  kwa kukiuka makubaliano kadha ya kuweka chini silaha ambayo yalifikiwa awali kati yake na serikali hiyo.

Upande wa Haftar mnamo Aprili 29 ulisema kuwa utasitisha mapigano katika kipindi cha mwezi wa mfungo kwa waislamu wa Ramadhan. ''Kamanda mkuu (Haftar) anatanganza kusitishwa kwa operesheni zote za kijeshi kutoka kwa upande wake,'' alisema Ahmad al-Mesmari, msemaji wa vikosi vya Haftar katika mji wa Benghazi ulioko mashariki mwa nchi hiyo.

Wito wa Haftar ulijiiri baada ya serikali ya GNA inayoungwa mkono na Uturuki kuvifurusha vikosi vya mbabe huyo wa kivita  kutoka katika ngome zake mbili zilioko magharibi mwa Tripoli.

Vikosi vya Haftar vimekuwa vikiendeleza operesheni za kijeshi kwa zaidi ya mwaka moja sasa kutaka kuudhibiti mji wa Tripoli. Mahasimu wa Haftar wanamtuhumu kwa kutaka kuanzisha utawala mpya wa udikteka wa kijeshi nchini Libya.

Taifa hilo la kaskazini mwa Afrika lenye utajiri mkubwa wa mafuta limegubikwa katika ghasia tangu mwaka 2011, alipoondolewa madarakani kiongozi wa mda mrefu Muammar Gaddafi.

Libyen Tripoli 2019 | Kämpfer der GNA
Mwanajeshi wa serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNA), akiwa katika makabiliano na vikosi vya Haftar katika mji wa Al-Yarmook mashariki mwa LibyaPicha: picture-alliance/Xinhua News Agency

Mnamo Aprili 24 Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na nchi nyingine mbali mbali zilitoa wito kwa pande zinaozozana nchini Libya kuweka chini silaha katika kipindi cha mfungo wa Ramadhan ambao ulianza siku hiyo hiyo.

Serikali ya GNA ilionya katika taarifa yake kuwa itandelea kuchukua hatua halali za kujilinda kwa kuyashambulia makundi yanotishia usalama wake. Kwa kuungwa mkono na Uturuki, serikali hiyo sasa imezingiria ngome kubwa ya Haftar katika mji wa Tarhuna uliopo umbali wa kilomita 80 Kusini mashariki mwa Tripoli.

Vikosi vya Umoja wa Mataifa Kulinda Amani nchini Libya (UNSMIL) mnamo Aprili 30  vilitoa tena wito kwa pande hasimu kumaliza uhasama ili kuwezesha mamlaka kushughulikia tishio la janga la COVID-19 na kueleza  wasiwasi wake kuhusu mashambulizi ambayo yamegahrimu maisha ya raia wa kawaida.

 Kulingana na takwimu za UNSMIL, watu 64 wameauwa katika mashambulizi hayo na wengine 134 kujeruhiwa tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi kufikia Machi 31. Tangu kuzuka kwa mapaigano kati ya vikosi vyenye utwiifu kwa Haftar na serikali ya GNA, makubaliano ya usitishwaji wa vita yamekiukwa mara kwa mara, kila upande ukiuonyoshea kidole mwingine kwa kutoheshimu makubaliano ya kuweka chini silaha.

Vyanzo: AFPE/RTRE