Wagombea urais tisa ndio wametangaza kwamba wataandaa maandamano kupinga matokeo yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi na kumpa ushindi wa muhula wa pili rais Félix Tshisekedi.
Miongoni mwa wagombea hao Moïse Katumbi, Martin Fayulu na Denis Mukwege.
Wanasiasa hao walikataa kufikisha malalamiko yao mbele ya mahakama ya katiba ambayo wanadai ni ya ukabila na inatumiwa na mamlaka pamoja na jamii ya raïs Tshisekedi.
Badala yake, wamechagua njia ya kuandamana katika barabara zote za Kongo.
Serikali yasema haitavumilia maandamano ya kupinga matokeo
Hata hivyo serikali tayari imewaonya ikisema itakabiliana na yeyote atakayejaribu kuvuruga hali ya utulivu nchini.
Hayo yameelezwa na Patrick Muyaya ambaye ni msemaji wa serikali ya Kongo.
"Tabia nzuri ingelikuwa ni kusubiri matokeo ya muda halafu kufikisha malalamiko yao mbele ya mahakama. Sasa wanapokataa kujielekeza mahakamani watakwenda wapi ? Sisi wakati wa baraza la mawaziri, rais alituamuru wazi kushughulika na mambo ya serikali na kuwa na uhakika kwamba utulivu haujavurugwa." amesema afisa huyo wa serikali ya Kongo.
Baadhi ya mashirika ya kiraia pia yanaunga mkono msimamo huo wa upinzani yakiamini kuwa uchaguzi mkuu wa Disemba 20 uligubikwa na visa vya udanganyifu na hivyo matokeo yake sio halali.
Mashirika hayo pia yameeleza utayari wao wa kuandamana pamoja na wafuasi wa upinzani.
Wachambuzi wakosoa msimamo wa awali wa upinzani
Baadhi ya wachambuzi wanaeleza kwamba upinzani ulifanya makosa kukubali kushiriki uchaguzi ambao tangu mwanzo wa mchakato, ulikuwa umeonyesha dalili nyingi za udanganyifu.
Profesa Antoine Lokongo ambaye ni mhadhiri wa chuo kikuu cha Joseph Kasavubu amesema "Viongozi wa upinzani huo walikuwa wakiwaza labda wangelifaulu kuboresha mchakato ambao tayari ulikuwa umeharibika. Walikuwa wakitarajia kuwa na wabunge pamoja na maseneta. Lakini bunge hilo litakuwa ni la wafuasi wa Tshisekedi tu yaani nafasi zitakuwa tu kwa vyama vya utawala."
Baada ya tume huru ya uchaguzi Ceni kumtangaza rais Tshisekedi mshindi kwa kupata asilimia 73 ya kura, tume hiyo imewataka wagombea ambao hawajaridishwa na matokeo hayo kuwasilisha malalamiko yao mbele ya korti ya katiba kufikia leo jioni.
Korti hiyo ina muda wa siku saba ili kusikiliza malamiko hayo kabla ya kutoa uamuzi wa mwisho.