Serikali ya Ethiopia yadai kuchukua udhibiti wa Alamata
23 Desemba 2021Kitengo cha mawasiliano cha serikali ya Ethiopia kimesema jeshi la serikali pamoja na vikosi vya usalama vya eneo la Amhara vimechukua udhibiti wa mji wa Alamata na kusisitiza kwamba mapigano yataendelea.
Hiyo ni mara ya kwanza kwa wanajeshi wa serikali kupiga hatua ndani ya jimbo la Tigray lililokumbwa na vita kwa muda mrefu.
Baada ya kuudhibiti mji huo wa Alamata, serikali imesema vikosi vyake vinaelekea katika wilaya ya Abergele, ilioko pia katika jimbo la Tigray.
Hata hivyo, wapiganaji wa chama cha ukombozi wa watu wa Tigray, TPLF waliotangaza kujiondoa kutoka maeneo ya Amhara na Afar wiki hii na kutoa wito wa kusitishwa kwa mapigano, hawakujibu madai hayo ya serikali.
Soma pia: Ethiopia yaitaka Marekani kuacha kusambaza taarifa za uwongo
Kujiondoa kwa wapiganaji wa TPLF kutoka Amhara na Afar kuliongeza matumaini ya kuwepo mazungumzo ya kumaliza vita hivyo vilivyodumu miezi 13 ambavyo vimegharimu maisha ya maelfu ya watu na kusababisha mzozo mkubwa wa kibinadamu kando na kuwaacha maelfu ya wengine wakikabiliwa na baa la njaa.
Katika barua kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wiki hii, kiongozi wa chama cha ukombozi wa watu wa Tigray Debretsion Gebremichael alisema, anatumai kujiondoa kwa wapiganaji wa kundi hilo kutafungua fursa ya kupatikana amani.
Hata hivyo, mnamo siku ya Jumatatu serikali ilipuzilia mbali tangazo la TPLF la kujiondoa kutoka maeneo ya Amhara na Afar, badala yake ikidai tangazo hilo lilikuwa njia tu ya kuficha ukweli kwamba wapiganaji hao walikuwa wamezidiwa mbinu.
Soma pia: Amnesty: Wapiganaji wa Tigray walibaka, kupora na kuwapiga wanawake
Pande zote mbili zimekuwa zikidai kumiliki maeneo kadhaa katika miezi ya hivi karibuni, hata wakati mmoja wapiganaji wa TPLF wakijipiga kifua na kudai kuukaribia mji mkuu wa Addis Ababa lakini tangu wakati huo, Waziri Mkuu Abiy Ahmed ambaye ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel ya mwaka 2019, mnamo mwezi uliopita alitangaza kujitosa katika uwanja wa mapambano ili kukabiliana na waasi hao.
Kulingana na chombo cha habari cha serikali, serikali ya mjini Addis Ababa imedai kuchukua tena udhibiti wa miji muhimu iliyokuwa mikononi mwa wapiganaji waasi.
Vita hivyo vilivyozuka Novemba mwaka uliopita, vinatishia kusambaratisha moja ya mataifa yenye idadi kubwa ya watu duniani wakati hatma ya watu wapatao milioni 110 ikiwa njia panda.