1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroColombia

Serikali, waasi nchini Colombia kurejea mezani kusaka amani

10 Septemba 2024

Serikali ya Colombia na kundi kubwa la wapiganaji wa msituni wametangaza kwa pamoja kwamba watarejea kwenye meza ya mazungumzo ya kutafuta amani yaliyokwama tangu mwezi Julai.

https://p.dw.com/p/4kRVT
Colombia| FARC
Waliokuwa waasi wa kundi kubwa la wapiganaji wa msituni nchini Colombia la FARC wakiwa chini ya ulinzi wa jeshi la taifa.Picha: AP

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa jana Jumatatu serikali na kundi la waasi la Segunda Marquetalia wamesema watafanya mazungumzo yao mjini Havana nchini Cuba bila kutaja tarehe rasmi ya kuanza kwake.

Kundi la Segunda Marquetilia, ambalo ni la wapiganaji waliojitenga kutoka jeshi la msituni la waasi wa FARC lililovunjwa rasmi mwaka 2017, lilitangaza mwezi Juni kuweka chini silaha kupisha mazungumzo.

Lakini mashauriano hayo yalisambaratika mwezi uliofuata wa Julai na kundi hilo linailaumu serikali kwa kushindwa kufuta waranti wa kuwakamata viongozi wake.

Mkataba wa amani wa mwaka 2016 uliofanikisha kuvunjwa kwa jeshi la msituni la FARC ulitajwa kuwa hatua ya kihistoria ya kumaliza mapigano yaliyodumu kwa miongo kadhaa nchini Colombia.

Hata hivyo makundi mawili yaliasi makubaliano hayo na yanaendelea kupambana na vikosi vya serikali ya Colombia kwenye maeneo makubwa ya nchi hiyo.