Serikali mpya ya muungano imeapishwa Palestina
2 Juni 2014Rais Abbas aliyesimamia kuapishwa kwa mawaziri wapya wa serikali hiyo ya muungano ,hafla iliyofanyika katika ikulu ya rais mjini Ramallah amesifu kuungana kwa Fatah na mahasimu wake Hamas ambao wamekuwa wakitawala ukanda wa Gaza na kuitaja hatua hiyo kama mwisho wa mgawanyiko mkali na saa nyingine uliosababisha umwagikaji wa damu ambao umeathiri mustakabali wa Palestina.
Hamas pia imesifu kuundwa kwa serikali hiyo mpya na kuitaja inayowawakilisha wapalestina wote na ni ukurasa mpya katika mahusiano kati yake na Fatah.
Makubaliano yazaa matunda
Mawaziri wapya chini ya serikali hiyo ya muungano wamekula viapo kwa kuweka mikono yao juu ya Koran au bibilia.Hii ndiyo serikali ya kwanza ya muungano kuingia madarakani nchini humo katika kipindi cha miaka saba, matokeo ya kwanza ya makubaliano ya maridhiano yaliyotiwa saini mwezi Aprili mwaka huu.
Mapema hii leo, mzozo kuhusu ni nani atakayeshikia wadhifa wa waziri anayehusika na wafungwa ulizusha hofu kuwa huenda kutangazwa kwa serikali hiyo ya muungano kungecheleweshwa lakini suala hilo lilitatuliwa baada ya pande zote mbili kukubaliana kuwa wizara hiyo itakuwa chini ya waziri mkuu Rami Hamdallah ambaye pia atashikilia wadhifa wa waziri wa mambo ya ndani.
Baraza hilo jipya lina mawaziri kumi na saba wote wakiwa wataalamu wasioegemea vyama vya kisiasa na serikali hiyo mpya haitakuwa na mamlaka ya kisiasa.
Pande zote kuheshimu misingi ya utawala
Serikali hiyo ina wanawake watatu na mawaziri watano kutoka Gaza.Rais Abbas ameahidi kuwa serikali hiyo itaheshimu misingi iliyowekwa na pande nne zinazosimamia kutafutwa kwa amani Mashariki ya kati nayo ni kuitambua Israel,kupinga ghasia na kuzingatia makubaliano yote ambayo yapo.
Chini ya makubaliano hayo, chama cha ukombozi wa Palestina PLO kilikubali kushirikiana na Hamas kuunda serikali ya muda ya wataalamu ambao wataandaa chaguzi ambazo zimecheleweshwa kwa muda mrefu.
Israel imekasirishwa na hatua hiyo ya Rais Abbas kukubali kuwa na serikali ya muungano na Hamas,kundi ambalo Israel,Marekani na Umoja wa Ulaya imeliorodhesha kama kundi la kigaidi.
Hapo jana waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Marekani John Kerry alimpigia simu Abbas kuelezea wasiwasi wake kuhusu wajibu wa Hamas katika serikali.
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu hapo jana aliitaka jumuiya ya kimataifa kutokuwa na haraka katika kuitambua rasmi Palestina baada ya kuungana na Hamas na jana usiku baraza la mawaziri la Israel lilikutana kujadili serikali hiyo mpya ya Palestina na kutilia mkazo maamuzi waliyofikia mwezi Aprili ya kusitisha mazungumzo ya kutafuta amani kati ya Israel na Palestina kufuatia kujumuishwa kwa Hamas serikalini.
Mwandishi:Caro Robi/afp/dpa
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman