1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sera ya wakimbizi ilivyoijengea Ujerumani sifa nje

23 Agosti 2016

Sera za Ujerumani kuhusu wakimbizi zilipamba vichwa vya habari duniani kote mnamo mwaka wa 2015 na ulimwengu umekuwa ukifuatilia tangu wakati huo. Ni namna gani mgogoro wa wakimbizi umeijenga sifa ya Ujerumani nje?

https://p.dw.com/p/1JnFt
NATO Gipfel Polen Obama Merkel Press Office (BPA)
Kansela Merkel akiwa kwenye mkutano na Rais wa Marekani Barack Obama nchini Poland.Picha: Getty Images/Bundesregierung/G. Bergmann

Mwaka mmoja umepita tangu Ujerumani ilipofungua milango kwa maelfu ya wakimbizi na Kansela Angela Merkel kutamka maneo yake yaliojizolea umaarufu - Wir schaffen das. Tunaweza kulimudu hilo.

Wakosoaji wake nyumbani wamezidi kupaza sauti katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita wakiwa na ushahidi kwamba wakimbizi wameuongezea uzito mfumo, vurugu za makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia zimekuwa mbaya zaidi na ugaidi wa makundi ya itikadi kali za Kiislamu pia umeikumba Ujerumani.

Lakini ni jinsi gani mgogoro wa wakimbizi umeiathiri sifa ya Ujerumani kimataifa kama mshirika imara, taifa kubwa kiuchumi na nchi iliyo na historia ya matatizo?

Unafiki wa Ulaya

Ulaya ilikaa na kutazama wakati mgogoro wa wakimbizi ukifukuta kwa kipindi cha miaka kadhaa wakati machafuko na umaskini uliokithiri katika kanda ya Mashariki ya Kati, Asia ya Kati na Afrika vikiwalaazimu watu kuchukuwa hatua za kutotumainika katika kutafuta mahala salama. Majira ya kiangazi mwaka 2015 ndiyo kilikuwa kilele cha yote hayo.

Berlin Bundeskanzleramt Blumenstrauß Blumenstrauß für Angela Merkel
Machi 8, 2016 watu mashuhuri zaidi ya 100 waliandika barua ya wazi na kuipeleka pamoja na maua ofisini kwa kansela wakimshukuru kwa matashi ya "Wir Schaffen Das."Picha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenk

Ripoti za mara kwa mara za wahamiaji kufariki baharini na ardhini, zikijumlishwa na ukiukaji wa haki za wahamiaji uliokuwa ukifanywa na Hungary viliisukuma Ujerumani, kwa kushirikiana na Austria, kusitisha utekelezaji wa mkataba wa Dublin kwa wakimbizi wa Syria Agosti mwaka jana. Hatua hiyo iliwaweka huru Wasyria kutokana na mchakato wa hifadhi katika nchi ya Umoja wa Ulaya wanakoingilia; ilionekana pia kama ishara ya kuwakaribisha wakimbizi kila mahala.

Heshima ya Ujerumani ikaimarika katika kanda ya Mashariki ya Kati. Kulingana na Mehran Kamrava, mkuu wa kituo cha masuala ya kimataifa na kikanda katika shule ya huduma za nje ya Chuo Kikuu cha Georgetown nchini Qatar, mataifa ya Ulaya yanazingatiwa mara nyingi kuwa wanafiki wanaoihubiria Mashariki ya Kati kuhusu haki za binaadamu.

Kwa kuwakaribisha wakimbizi, Kamvara anasema hatua hiyo iliiondolea makali hoja ya unafiki, angalau kwa Ujerumani. Lakini Ibrahim Awad, anaeongoza kitu cha utafiti wa wakimbizi na uhamiaji katika Chuo Kikuu cha Marekani mjini Cairo, anasisitiza kuwa wapo wanaodhani kwamba Ulaya inautia chumvi mmiminiko wa wakimbizi barani humo.

Wasyria milioni 11 wamepoteza makaazi yao tangu 2011, milioni sita kati yao ni wakimbizi wa ndani. Uturuki kwa sasa inawahifadhi Wasyria milioni 2.5, ikifuatiwa na Lebanon iliyowapokea wakimbizi milioni 1.1, Jordan imepokea wakimbizi 635,000 na Misri 117,000.

Inahitaji zaidi

Sifa ya Ujerumani pia iliimarika Asia ya Kati na Afrika - kanda ambazo zimechangia pakubwa katika idadi ya wakimbizi. Hususani barani Afrika, sera za ukimbizi za serikali mjini Berlin zimebadilisha pakubwa mtazamo jumla kuhusu Ulaya.

"Wazo la ngome ya Ulaya limekuwa kwamba Ulaya itafanya kila kitu kuwazuwia wahamiaji," alisema Liesl Louw-Vaudran kutoka kituo cha masuala ya usalama kilicho na makao yake Afrika Kusini katika mahojiano na DW. Aliongeza kuwa kinachoshuhudiwa kwa sasa ni mabadiliko kutoka kila kitu tulichokijua hadi sasa kuhusu uhamiaji na Ulaya.

BdT Deutschland Rügen Bauzaun Wir schaffen das nie Frau Merkel
Lakini ujumbe mwingine ulikuwa unapingana na tamko la kansela ukisema, "Hatuwezi".Picha: picture-alliance/dpa/S. Sauer

Lakini ukosoaji wa ufungaji mipaka unagusa shauku ya muda mrefu kwamba Ulaya - hasa watawala wa zamani wa kikoloni waliochukuwa rasilimali za Afrika - wafanye zaidi kwa ajili ya uhamiaji uliyoratibiwa. Louw-Vaudran anaongeza kuwa hata hivyo, kuwa serikali za Kiafrika zinazounga mkono hoja hii, kamwe haziwezi kukiri kuwa zinahimiza uhamiaji kama mfumo wa kuingiza kipato.

Ujerumani, mtulizaji

Ishara ya kibinaadamu ya Ujerumani ilikuwa na athari mbili kuu kuhusu sifa yake na washirika wake muhimu zaidi: Ilipata heshima kama nchi yenye "mamlaka ya kimaadili" na kuonyehsa zaidi jukumu lake la uongozi katika Umoja wa Ulaya. Suala la iwapo hilo ni jambo chanya linategemea na nchi yenyewe.

China - ambayo imejenga uhusiano wa karibu wa kidiplomasia na serikali ya Kansela Merkel - imeutazama uamuzi huo uliyofanywa na mshirika wake muhimu zaidi wa kibiashara katika Umoja wa Ulaya kwa mvuto na kusita.

Wasiwasi mkuu wa Beijing ni uwiano kati ya sera ya ukimbizi na usalama dhaifu, anasema Xuewu Gu kutoka kituo cha masuala ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Bonn. China inaichukulia Ujerumani kama mdau muhimu katika kuhakikisha mwambatano wa Ulaya na hivyo, Ulaya iliyo imara ambayo inaweza kusaidia kudhoofisha udhibiti wa Marekani.

Utawala wa Obama pia unaitazama Berlin kama mshirika wake wa kutegemewa zaidi barani Ulaya katika wakati ambapo rais huyo wa Marekani anahitaji "mwambatano wa mataifa ya Magharibi ili kutekeleza hatua nyingi za kisera zinazohitaji kuchukuliwa," anasema Cathryn Clüver, mkurugenzi wa mradi wa "Future Diplomacy" wa Chuo Kikuu cha Havard.

Siyo tu Obama ameisifu Ujerumani kwa "kuwa katika upande sahihi wa historia," lakini pia umma wa Wamarekani unathamini pakubwa ishara yake ya kibinaadamu, ukiona mgongano na historia yake ya zamani ya uhamiaji.

Lakini yanapokuja makubaliano ya wakimbizi na Uturuki, China na Marekani zinatilia mashaka. Gu anasema Beijing inaona hatua ya Merkel kushinikiza makubaliano hayo kuwa jambo "lisilola busara."

Deutschland Karneval Motivwagen Vorschau Köln
Ubunifu mbalimbali umetumiwa kuakisi tamko la "Wir schaffen das" kama inavyoonekana kama picha hii.Picha: picture-alliance/dpa/O. Berg

Uzuri, ubaya na Merkel wa uongozi wa Ujerumani

Kwa ulimwengu, Merkel ni mwanasiasa wa kuvutia ambaye jina lake limegeuka kuwa na maana sawa na Ujerumani. Kwa baadhi, Merkel ndiye binti wa mhubiri mwenye dhamira, mfizikia makini, "mtawala poa wa Ulaya." Kwa wengine lakini, ni mpumbavu alielewa madaraka.

Serikali zake tatu zimetengeneza sifa ya Ujerumani katika Umoja wa Ulaya katika kipindi cha muongo mmoja uliopita. Akikabiliwa na uchaguzi mkuu mwaka 2017, muhula wake wa tatu madarakani huenda ukawa wa mwisho kwake kutegemea na matukio katika mgogoro huu wa wakimbizi.

Mwaka uliopita wa hisia za uhamiaji, ugaidi na itikadi kali za mrengo wa kulia, pamoja na kura ya maoni ya Brexit, umeichora Berlin kama msimamizi wa migogoro mbalimbali, ikiwakasirisha baadhi na kuwafurahisha wengine.

Profesa wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Sorbonne Anne-Laura Delatte anasema Umoja wa Ulaya unaoitegemea zaidi Ujerumani unazua maswali makubwa zaidi kuhusu ufanisi wa umoja huo, na hivyo kutilia mkazo ukosoaji wa mkakati wa Merkel wa kushughulikia migogoro mbalimbali inaolikumba bara hilo.

"Hatupaswi kuzungumzia kuhusu Ujerumani kufanya maamuzi kwa ajili ya Ulaya. Tunapaswa kuzungumzia kundi la mataifa yakifanya maamuzi wenyewe," Delatte aliiambia DW.

Lakini bado kuna swali hata kubwa zaidi, anasema Kaypso Nicolaidis, aneongoza masuala ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Oxford. Je, kiongozi anaesita Ujerumani inaweza kujiafikisha vyema na sifa yake ya kimataifa kama taifa kubwa, mdau muhimu wa kimataifa, na bado ikatafuta sauti stahiki kwa kuzingatia historia yake ya unazi?

"IKiwa kuna nchi moja inayoamini kuwa ni shida kuona kujitokeza tena aina fulani ya Ujerumani barani Ulaya, ni Ujerumani yenyewe," anasema Nicolaidis.

Mwandishi: Kathleen Schuster/DW

Tafsiri: Iddi Ssessanga

Mhariri: Yusra Buwayhid