Sera ya Trump Mashariki ya Kati yashusha heshima ya Marekani
18 Januari 2018Mwanzoni mwa mwezi Desemba mwaka jana makamu wa rais wa Marekani Mike Pence alifuta ziara yake katika eneo la mashariki ya kati. Sasa amepanga tena kuifanya ziara hiyo.
Wakati ule hali ilikuwa mbaya sana, baada ya rais wake Donald Trump kuutambua mji wa Jerusalem kama mji mkuu wa Israel, na kutangaza azma ya kuuhamishia ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv kwenda Jerusalem.
Baada ya tangazo hilo heshima ya Marekani katika eneo kubwa la mataifa ya Kiarabu iliporomoka. Hususan kwa Wapalestina ambao walijihisi kwamba maslahi yao hayakuangaliwa. Kwa hiyo ilionekana mjini Washington kama ilivyo katika miji mikuu ya mataifa ya mashariki ya kati kuwa ni busara kwanza kuiahirisha ziara hiyo hadi wakati mwingine baadaye.
Ziara yaangukia mwaka mmoja wa Trump
Kwa hivi sasa hali imetulia na tarehe 19. Januari Pence anaanza ziara hiyo. Anatarajiwa kufika mjini Jerusalem, Cairo na kama ilivyokubaliwa atafika pia katika mji mkuu wa Jordan Amman.
Ziara hiyo ya makamu wa rais inaangukia katika siku ambayo kunaadhimishwa mwaka mmoja tangu utawala wa Trump kuingia madarakani, tarehe 20 Januari 2017.
Kimsingi anasema mtaalamu wa masuala ya mashariki ya kati Andre Bank kutoka katika taasisi ya utafiti wa masuala ya mashariki ya kati ya GIGA mjini Hamburg, kwamba Trump ana mwelekeo wake katika sera za mashariki ya kati, lakini sio kama watangulizi wake.
"Sioni tofauti kubwa katika nyanja zingine isipokuwa katika sera za mambo ya kigeni, ukilinganisha na maeneo mengine. Kwa kulinganisha na rais Obama kwa mfano katika sera kuelekea mashariki ya mbali , kumekuwa na mivutano zaidi, hususan China. Kwa upande wa Ulaya hali imekuwa mbaya zaidi tangu Trump kuingia madarakani.
Sera kuelekea Syria
Lakini kitu cha ajabu ni kwamba katika mashariki ya kati na hususan kuhusu Syria hakuna mengi aliyobadilisha, ukilinganisha na utawala wa Obama. Na inaonekana Marekani tayari inachukua sera ya kujiweka kando," anasema Bank.
Kuhusu Syria mtangulizi wa Trump, rais Barack Obama katika kipindi chake chote cha utawala alifuata njia ya kujizuwia. Katikati ya mwaka 2012 Obama alitoa onyo kali kwa serikali ya Syria.
Wakitumia gesi ya sumu dhidi ya mahasimu wake, itakuwa ni kuvuka 'mstari mwekundu'. Rais wa Syria Bashar al-Assad alionekana hakustushwa na kauli hiyo.
Hata baada ya kutokea mashambulizi ya gesi ya sumu Obama hakuchukua hatua, na badala yake aliwapa tu waasi silaha. Hata utawala wa Trump nao haukufanya chochote isipokuwa kufuata mfano wa Obama, kwa kupambana na kundi linalojiita Dola la Kiislamu.
Saudia yaafiki sera ya Trump
Waziri wa ulinzi wa Saudi Arabia na mwanamfalme Mohammed bin Salman kwa kuonesha wazi kuwapo karibu na Trump ameidhinisha sera zake.
Viongozi hao wawili wanaonesha kuaminiana, kwasababu ya wote wanamtazamo hasimu na Iran, ikiwa ni nchi yenye ushindani mkubwa nana Saudi Arabia kuwania ushawishi katika eneo la Mashariki ya Kati.
Rais wa Marekani, anasema mtaalamu wa masuala ya Saudi Arabia Sebastian Sons kutoka taasisi ya Ujerumani inayojishughulisha na masuala ya kigeni , na viongozi hao wana msimamo mmoja kuhusu mzozo wa Jemen.
Mwandishi : Knipp, Kersten / Sekione Kitojo
Mhariri: Gakuba, Daniel