Seoul yathibitisha kukamatwa wanajeshi wa Korea Kaskazini
12 Januari 2025Idara ya ujasusi ya Korea Kusini imethibitisha leo, kuwa Ukraine iliwakamata wanajeshi wawili wa Korea Kaskazini waliojeruhiwa wiki hii nchini Urusi, baada ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kusema wanahojiwa.
Taarifa ya idara ya ujasusi ya Korea Kusini NIS, imesema wanajeshi hao wa Korea Kaskazini, walikamatwa mnamo Januari 9 katika uwanja wa mapambano huko mkoani Kursk nchini Urusi.
Siku ya Jumamosi, Kyiv haikuwasilisha ushahidi wa moja kwa moja kwamba watu waliokamatwa walikuwa ni wanajeshi wa Korea Kaskazini, ingawa uthibitisho wa Korea Kusini unaongeza uzito wa madai ya Ukraine, huku Urusi na Korea Kaskazini zikiwa hazijatoa tamko lolote kuhusu suala hilo.
Ukraine, Marekani na Korea Kusini zimeishutumu Korea Kaskazini yenye silaha za nyuklia kwa kutuma zaidi ya wanajeshi 10,000 kuisaidia Urusi kupambana na Ukraine.