1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz, Habeck waelezea wasiwasi kuhusu Musk na AfD

4 Januari 2025

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na Makamu wake Robert Habeck wameelezea wasiwasi juu ya bilionea wa Marekani Elon Musk kuunga mkono chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD kabla ya uchaguzi wa Februari.

https://p.dw.com/p/4ooUa
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akizungumza kwenye ufunguzi wa wa kiwanda cha Tesla pamoja na Elon Musk mwaka wa 2022
Scholz (kushoto) amewahi kukutana na Musk mara moja pekee, kwenye ufunguzi wa kiwanda cha Tesla Ujerumani Machi 2022Picha: Patrick Pleul/dpa/picture alliance

Scholz, wa chama cha Social Democratic (SPD), ameliambia jarida la Stern katika makala iliyochapishwa Jumamosi, kwamba ingawa hajashtushwa na kauli za Musk dhidi yake na wanasiasa wengine wa Ujerumani, uungwaji mkono wa Musk kwa chama hicho cha mrengo wa kulia unatia wasiwasi zaidi.

Shirika la kijasusi la ndani la Ujerumani la BfV linakifuatilia chama cha kitaifa cha AfD kama kikundi kinachoshukiwa kuwa na itikadi kali za mrengo wa kulia, na mashirika kadhaa ya ngazi ya majimbo tayari yamekiorodhesha kuwa cha mrengo huo.

Habeck, mgombea wa chama cha Kijani katika uchaguzi ujao, amemuonya Musk, ambaye ni mfuasi mkubwa wa Rais mteule wa Marekani Donald Trump, dhidi ya kuingilia uchaguzi wa Ujerumani. Habeck amesema katika jarida la habari la Spiegel kuwa "Mchanganyiko wa utajiri mkubwa, udhibiti wa habari na mitandao ya kijamii, matumizi ya akili mnemba (AI) na nia ya kupuuza sheria ni shambulio la moja kwa moja kwa demokrasia ya Wajerumani."