Scholz atoa rai ya utulivu kumaliza mzozo wa kisiasa
9 Novemba 2024Akizungumza na waandishi habari mjini Budapest, Scholz amepuuza madai yanayotolewa na wanasiasa wenzake kwamba anaelenga kuuchelewesha uchaguzi kwa malengo ya kukamilisha kwanza vipaumbele vyake vya kisiasa.
Ujerumani ilitumbukia kwenye mzozo wa kisiasa mapema wiki hii kufuatia kusambaratika kwa serikali ya muungano wa vyama vitatu inayoongozwa na Scholz baada ya kiongozi huyo kumfuta kazi waziri wake wa fedha Christian Lindner.
Uamuzi huo ulimaanisha kwamba serikali ya Scholz imepoteza wingi wa viti bungeni na mwenyewe alipendekeza kuitishwa kura ya imani kwa serikali yake mnamo mwezi Januari na kisha uchaguzi wa mapema hapo mwezi Machi. Hata hivyo chama kikuu cha upinzani cha Christian Democratic Union CDU kinataka uchaguzi ufanyike mwezi Januari.