Scholz atoa mwito kwa Ujerumani kuungana kunusuru taifa
6 Septemba 2023Akizungumza katika bunge mapema leo, kansela Scholz ameutolea mwito muungano wa vyama tawala, upinzani wa kidemokrasia na mamlaka za manispaa kushirikiana ilikuondokana na ukiritimba, na kuepusha hali ya hatari na kukata tamaa ambayo imeenea katika taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya katika miaka ya hivi karibuni.
"Pendekezo langu linaelekezwa kwa wakuu 16 wa serikali za majimbo, kwa wasimamizi wa wilaya, kwa mameya kote katika Jamhuri yetu. Na pendekezo langu pia linaelekezwa kwa uwazi kwako, Bw Merz - kama kiongozi wa chama kikuu cha upinzani, ambacho kinabeba jukumu kubwa katika Bundesrat, katika majimbo na katika manispaa. Tunahitaji maonyesho ya kitaifa ya nguvu. Kwa hivyo tuunganishe nguvu!", alisema Kansela Scholz.
Kulingana na waraka wa serikali, mkataba huo unaweka malengo kadhaa ya kufikiwa kwa kushauriana na serikali zenye nguvu za majimbo ikiwa ni pamoja na michakato ya haraka ya mashauriano ya mtandaoni kwa ajili ya mashamba ya upepo na mitandao ya usafiri na data.
Scholz ajibu maswali bungeni: Kansela Scholz ajibu maswali ya wabunge, asema usalama ni suala lenye kipaumbele
Scholz amesema wananchi wanahitaji mwelekeo na maelewano ya ujasiri. Hilo ndiyo hitaji langu kwetu sote; vyama vya serikali ambavyo vimepaza sauti katika miezi ya karibuni na pia upinzani wa kidemokrasia, amesema kansela Scholz. Amesema hili ni jambo la msingi ili kukabiliana na wale aliosema wanataka kujinufaisha kisiasa kutokana na changamoto zinazoikumba serikali na kuzusha hofu, akimaanisha chama cha AfD, ambacho uchunguzi wa maoni unaonyesha umaarufu wake umeongezeka pakubwa hadi nafasi ya pili mbele ya chama cha Scholz cha SPD.
"Wananchi wengi wanajua kwamba wanaojiita 'Mbadala' kiuhalisia ni komando wa kubomoa - kikosi cha kuibomoa nchi yetu."
Som pia:Scholz asema umaarufu wa AfD ni "moto wa mabua"
Kansela Scholz amekataa wazo la mpango mpya wa kuchochea ukuaji wa uchumi unaopambana na mfumuko mkubwa wa bei, gharama za ufadhili na kushuka kwa mauzo ya nje, na kusema serikali tayari ilikuwa inawekeza fedha nyingi. Mpango wa bajeti ya mwaka 2024 unatazamiwa kuwekeza euro bilioni 58 kutoka kwenye mfuko wake wa tabianchi katika nishati ya haidrojeni, teknolojia ya chip na usafiri rafiki kwa mazingira, miundombinu ya kidijitali na ukarabati wa majengo.
Pia ilikuwa inawekeza euro bilioni 54 kutoka bajeti ya kawaida katika miundombinu ya reli, madaraja mapya, mtandao wa kasi zaidi wa intaneti, vituo vya malipo, makazi ya kijamii na uchumi wa kimazingira. Shirika la reli la Deutsche Bahn pekee lilikuwa limetenegwa euro bilioni 24 za ziada kwa uwekezaji katika miaka minne ijayo.