Scholz atembelea Solingen kulikofanyika shambulio la kisu
26 Agosti 2024Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ametoa heshima kwa wahanga wa shambulio la kisu katika jiji la Solingen. Maua, mishumaa na ujumbe wa maandishi vimetanda barabarani tangu siku ya Ijumaa usiku.
Solingen ni jiji lenye takriban watu 160,000, liko kati ya miji ya Duesseldorf na Cologne.
Mshukiwa ambaye ni raia wa Syria mwenye umri wa miaka 26 amewekwa kizuizini tangu Jumapili jioni anakabiliwa na tuhuma mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwa mwanachama wa kundi la kigaidi IS, na mauaji.
Soma Pia: Polisi ya Ujerumani yapata kifaa inachoshuku kimetumika katika shambulio la Solingen
Waendesha mashtaka wa Ujerumani wanaopambana na ugaidi wanamchunguza mtu huyo anayeitwa Issa al H.
Kundi la kigaidi la IS lilisema katika taarifa yake siku ya Jumamosi kwamba mmoja wa wanachama wake amefanya shambulio hilo ili "kulipiza kisasi" kwa niaba ya waislamu wa Palestina na wa kila mahali.
Mashambulio hayo yalifanyika siku ya ijumaa jioni, wakati wa tamasha katika jiji Solingen ililopo magharibi mwa Ujerumani. Watu watatu waliuawa, wengine wanane walijeruhiwa na wanne kati yao wakiwa katika hali mahututi.
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameyaelezea mashambulio hayo ya kisu kama uhalifu mbaya na amesema ni lazima nguvu kamili za sheria zitumike.
Kutokana na shambulio hilo baya la kisu katika mji wa Solingen, upande wa upinzani umeongeza shinikizo la kupinga wahamiaji, Friedrich Merz, kiongozi wa chama cha mrengo wa kulia cha Christian Democratic Union (CDU), ametoa wito wa kufanyika uchaguzi ili kusitisha mara moja upokeaji wa wakimbizi kutoka Syria na Afghanistan.
Waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la North Rhine Westphalia, Herbert Reul, liliko jiji la Solingen ametaka ukaguzi uimarishwe katika mipaka ya Ujerumani yote na hatua zichukuliwe za kuwakataa wakimbizi.
Soma Pia: Waziri wa ulinzi wa Ujerumani alaani shambulio la kisu Solingen
Mwanasiasa huyo wa kihafidhina amesisitizta kuwa ni muhimu sana kuchukua hatua za kupunguza wahamiaji. Amesema ni sahihi kuondolewa nchini Ujerumani wakimbizi ambao maombi yao hayajakubaliwa na hasa wa kutoka Afghanistan na Syria anakotoka mshukiwa wa mashambulio ya Solingen.
Katibu mkuu wa chama kinachotawala cha Ujerumani Social Democrats (SPD), Kevin Kühnert, amepinga wito wa upinzani.
Kikao maalum cha bunge kitafanyika katika Bunge la jimbo la NorthRhine Westphalia baadaye wiki hii kufuatia mashambulizi ya kisu katika mji wa Solingen, vyama vya (SPD) na (FDP) vimesema leo Jumatatu.
Vyanzo: DPA/AFP