1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Schalke yamtaka Uth arejee kutoka Cologne

2 Mei 2020

Klabu ya Schalke 04 inamtaka mshambuliaji wake Mark Uth ambaye amekuwa akiichezea Cologne kwa mkopo, arejee nyumbani kuimarisha kikosi msimu ujao.

https://p.dw.com/p/3bhWB
Fußball Bundesliga 1.FC Köln - VfL Wolfsburg Mark Uth
Picha: picture-alliance/augenklick/firo Sportphoto/R. Ibing

Schalke wanajiandaa kukamilisha muda wa mchezaji wake wa safu ya ushambuliaji Mark Uth katika klabu hasimu ya Cologne - labda pengine Cologne wawe wako tayari kulipa kitita kikubwa kuubadili mkataba wa mkopo kuwa wa kudumu.

"Tuna furaha kwa kazi nzuri ambayo Mark Uth ameifanya Cologne. Kwa jinsi mambo yalivyo sasa namtarajia atavaa tena jezi ya buluu ya kifalme msimu ujao," mkurugenzi wa michezo wa Schalke, Jochen Schneider, ameliambia gazeti la Bild toleo la Jumamosi (02.05.2020).

Uth ana mabao manne na pasi nne zilizosaidia mabao kutiwa kimyani katika mechi saba tangu alipojiunga na Cologne wakati wa kipindi cha mapumziko cha msimu wa baridi na kabla ya mlipuko wa janga la virusi vya corona kusababisha ligi kusitishwa, baada ya kutofunga bao nusu ya kwanza ya msimu alipokuwa Schalke.

Cologne wanaripotiwa wanamnyatia na wanataka sana kuurefusha mkataba wa mkopo au kuubadili uwe wa kudumu. Lakini kwa sababu ya janga la corona hawako tayari kulipa gharama ya euro milioni 10, kwa mujibu wa gazeti la Bild, lakini wanataka kutumia chini ya nusu ya kiwango hicho.

Timu ya Schalke, ambayo hali yake ya kifedha imezorota kwa kiwango kikubwa kutokana na gonjwa la COVID-19, hawatarajiwi kukubali kiwango kidogo cha fedha kwa ajili ya uhamisho na huenda wakamuona Uth kama mchezaji atakayeimarisha kikosi chao msimu ujao huku dirisha na soko la usajili na uhamisho likitarajiwa kuwa gumu.

(dpa)