Saudia na Iran zatakiwa kupunguza mvutano
11 Januari 2016Uturuki imesema mvutano wa kisiasa kati ya nchi hizo mbili hauwezi kuchangia amani katika kanda hiyo ambayo tayari inafanana na mahala pa hatari panapoweza kuripuka.Naibu waziri mkuu wa Uturuki Numan Kurtulmus ametowa kauli hiyo kwa kupitia mtandao wake wa Twitter ambapo amezitaka nchi hizo kufanya juhudi za kupunguza mvutano.
Naibu waziri wa mambo ya nje wa China Zhang Ming alipokuwa ziarani katika nchi hizo wiki iliopita pia amehimiza utulivu na kuzitaka zijizuwie na hatua zenye kuupallilia mzozo huo.
Ametala utatuzi wa tafauti zao ufanyike kwa kupitia mazungumzo na kuchukuwa hatua za pamoja kuboresha uhusiano kati ya nchi hizo.Pia ameelezea matumaini yake kwamba nchi hizo zitashirikiana katika kulinda amani na utulivu Mashariki ya Kati.
China yahimiza utulivu
China inaitegemea Mashariki ya Kati kwa mafuta yake lakini kwa muda mrefu imekuwa haijishughughulishi sana katika juhudi za kidoplomasia na mizozo mengine katika kanda hiyo na ni hivi karibuni tu imeanza kutanuwa dhima yake hususan katika suala la mzozo wa Syria.
Mwezi uliopita ilikuwa mwenyeji katika mikutano na wajumbe wa serikali ya Syria halikadhalika wapinzani kutafuta suluhisho la kisiasa kwa mzozo wa nchi hiyo licha ya kwamba mara nne ilipiga kura ya turufu dhidi ya maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yaliyokusudia kuutafutia ufumbuzi mzozo huo la karibuni kabisa lilikuwa lile la kutaka ufanyike uchunguzi kuhusu uhalifu wa kivita uliofanyika nchini humo.
Nchi nyengine vigogo katika ulimwengu wa Kiislamu za Pakistan na Algeria tayari zimejiunga na Umoja wa Ulaya na Marekani kutowa wito wa usuluhishi kutokana na hofu kwamba mzozo huo utakwamisha juhudi za kutafuta amani nchini Yemen na Syria ambapo mataifa hayo mawili makubwa katika Ghuba yanaziunga mkono pande mbili tafauti zinazohasimiana katika mizozo ya nchi hizo.
Mazungumzo ya Syria ,Yemen kutoathiriwa
Staffan de Mistura mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na mzozo wa Syria. amesema "Mojawapo ya wasi wasi wangu mwenyewe lilikuwa ni suala la iwapo mvutano uliopo hivi sasa kati ya Saudi Arabia na Iran unavyoweza kuathiri au kutoathiri kuanza kwa mazungumzo ya Syria mjini Geneva."
Nchi zote mbili Saudi Arabia na Iran zimemuhakikishia mjumbe huyo kwamba mzozo wao huo hautoathiiri mazungumzo ya mmzozo wa Syria huko Geneva wala mazungumzo ya mzozo wa Yemen yaliopangwa kufanyika Vienna.
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu hapo jana ilikutana mjini Cairo kikao cha dharura na kuishutumu Iran kwa kuingilia kati masuala ya nchi nyengine Mashariki ya Kati na kuyumbisha usalama wa eneo hilo.
Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef