Saudia yasema Al Otaibi aliyekamatwa Ufaransa sio mtuhumiwa
8 Desemba 2021Maafisa wa Ufaransa wanatafuta uthibitisho kumtambua mtu aliyekamatwa jana Jumanne akishukiwa kuwa mtuhumiwa mkuu katika mauaji ya mwaka 2018 ya mwandishi habari wa Kisaudi Jamal Khashoggi.Hatua ya Ufaransa inachukuliwa baada ya Saudi Arabia kusisitiza kwamba aliyekamatwa sio mtuhumiwa anayetafutwa.
Baada ya mtuhumiwa raia wa Saudi Arabia Khaled Aedh Al-Otaibi kukamatwa jana katika uwanja wa ndege wa Roissy majira ya asubuhi wakati akitaka kupanda ndege kuelekea Saudi,mjumbe wa Umoja wa Mataifa wa shirika la kutetea haki za binadamu la kimataifa Amnesty International anayehusika na suala la kesi kuhusu mauaji ya Khashoggi , Agnes Callamard alisema.
"Mtu aliyekamatwa ni sehemu ya kundi lililohusika kupokea mwili au sehemu za mwili wa bwana Khashoggi . Anaaminika kuwa mmoja wa wale waliotoa uamuzi kuhusu wapi mwili huo utafichwa. Kwa hivyo mtu huyu anaweza kuwa na taarifa muhimu sana katika kuitafuta haki na kwa familia''
Al-Otaibi alikamatwa baada ya kutolewa ujumbe wa tahadhari na polisi ya kimataifa Interpol kwa niaba ya Uturuki wakati alipokuwa akipita kwenye sehemu ya ukaguzi wa pasipoti. Lakini ubalozi wa Saudi Arabia mjini Paris jana jioni ulitowa taarifa ukisema mtu huyo aliyekamatwa hahusiki kwa namna yoyote katika kesi hiyo inayozungumziwa,na kutaka aachiwe mara moja.
Ingawa inaelezwa kwamba Al Otaibi ni miongoni mwa watu waliokuweko katika ubalozi mdogo wa saudia huko Istanbul Uturuki siku Khashoggi alipoingia kwenye ubalozi huo na kutokomea hukohuko.
Lakini pia inaelezwa kwamba ni mmoja wa walinzi wa utawala wa kifalme wa Saudi na inaaminika ni miongoni mwa makommando waliomuua mwandishi habari huyo mkosoaji wa utawala wa Saudia katika operesheni ambayo huenda ilifadhiliwa na mwanamfalme Mohammed bin Salmane.
Hata hivyo baada ya kukamatwa Alotaibi chanzo kimoja cha usalama ndani ya Saudi Arabia kilisema kwamba Khaled Alotaibi ni jina maarufu sana katika nchi hiyo ya kifalme,kwa maana ya kwamba kuna watu wengi wanaoitwa jina hilo,na kwamba huyu aliyekamatwa sio mtu aliyekusudiwa,na huyo wafaransa wanayemdhania kimsingi yuko jela nchini Saudi Arabia pamoja na watuhumiwa wengine katika kesi hiyo ya Khashoggi.
Mwandishi: Saumu Mwasimba/afpe
Mhariri: Daniel Gakuba