Satelaiti kuleta tumaini la intaneti katika nchi maskini
6 Machi 2023Hata hivyo satelaiti zinazorushwa juu kidogo angani huweza kuwapa mamilioni ya watu matumaini, hususan wanaoishi vijijini barani Afrika.
Kampuni kubwakubwa za kiteknolojia na mawasiliano ikiwemo Microsoft zimeahidi kuwasaidia watu wanaosongwa na intaneti zinazosuasua, ili waingie katika enzi mpya ya muunganisho mitandaoni.
Satelaiti itakuwa na umihumu mkubwa kufanikisha lengo hilo, wakati kampuni pinzani zikirusha juu angani maelfu ya vidude hivyo vipya na vya kisasa vya kuimarisha intaneti.
Kuzinduliwa kwa satelaiti hizo, huenda kutaleta mabadiliko kwa haraka na kuimarisha matumaini ya Afrika. Wataalamu wa kiteknolojia waliahidi hilo kwenye mkutano wa kilele wa nchi maskini mjini Doha, Qatar.
Microsoft kuwaunganisha watu milioni 100 na intaneti
Kusambazwa kwa satelaiti hizo kutakuwa na umuhimu kwa kampuni ya Microsoft kuwaunganisha watu milioni 100 na mtandao wa intaneti ifikapo mwaka 2025, kama ilivyoainishwa kabla ya mkutano huo wa kilele.
Mnamo mwezi Desemba kampuni ya Microsoft ilitangaza awamu ya kwanza ya mradi huo kuwalenga watu milioni tano barani Afrika na imeahidi kuwaunganisha watu wengine milioni 20.
Watu milioni tano waliolengwa kwenye awamu ya kwanza watahudumiwa na kampuni ya Viasat. Mojawapo ya kampuni zinazosambaza satelaiti angani ili kushindana na intaneti inayosambazwa kwa njia ya waya wa chini ya bahari.
Kampuni ya X yake Elon Musk na Starlink pia zinapanga kurusha satelaiti zao kwenye orbiti umbali wa kati ya kilomita 400 na 700 angani kutoka ardhini.
Kwa sasa ni asilimia 36 pekee ya watu bilioni 1.25 katika nchi masikini kote ulimwenguni huweza kutumia intaneti. Hii ni tofauti na Ulaya ambapo, zaidi ya asilimia 90 ya watu katika nchi za Umoja wa Ulaya wana intaneti.
Chama cha Kimataifa cha Mawasiliano (ITU) kimelaani ukosefu huo wa usawa kuhusu upatikanaji wa intaneti, kikisema pengo hilo limezidi kutanuka katika muda wa muongo mmoja uliopita.
Guterres: Nchi maskini zaachwa nyuma kwenye mapinduzi ya kidijitali
Ukosefu wa usawa katika upatikanaji wa intaneti, ulikuwa suala muhimu la mazungumzo kwenye mkutano wa kilele wa nchi maskini mjini Doha, ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, aliwaambia viongozi kwamba wanaachwa nyuma katika kile alichokitaja kuwa ‘mapinduzi ya kidijitali'.
Upungufu wa huduma za kidijitali ni mkubwa sana katika baadhi ya nchi za Afrika ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambako katika takriban idadi jumla ya watu wake wote milioni 100, ni robo pekee ndio wanaweza kujiunga na intaneti.
Japo intaneti hupatikana katika miji mikubwa kama Kinshasa, maeneo mengi ya vijiji na ambayo yamezongwa na machafuko ya waasi kwa zaidi ya mmiongo miwili, yamesalia kuwa jangwa kuhusu masuala ya kidijitali.
Rais wa kampuni ya Microsoft, Brad Smith aliliambia shirika la habari la AFP kwamba wakati alipoona pendekezo la watu milioni 20 mwaka uliopita, aliuliza kama kweli ingewezekana, lakini sasa anaamini inawezekana.
Gharama ya teknolojia yashuka
Amesema gharama za teknolojia zimeshuka pakubwa na zitaendelea kushuka, na hiyo ni sehemu ya kile kinachofanya kusonga upesi kufikia idadi hiyo kubwa ya watu.
Ameongeza kuwa nchi barani Afrika, zina nafasi kupiga hatua mbele kuliko nchi nyingine linapokuja suala la udhibiti wa kitu kama mawasiliano bila kutumia nyaya.
Kulingana na Brad, kwa kutumia satelaiti kusambaza intaneti, wanaweza kuwafikia watu wengi zaidi kuliko wakitumia mifumo mingine ya kiteknolojia ya nyaya ambayo imekuwa ikitumika miaka mitano, kumi au kumi na mitano iliyopita.
Chanzo: AFPE