1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

191211 Zehn Jahre Euro-Bargeld

Mohammed Khelef2 Januari 2012

Katikati ya Disemba 2001, raia wa nchi 12 za Ulaya waliishika sarafu ya euro mikononi mwao kwa mara ya kwanza, baada ya mashaka ya namna ambavyo raia hao wangeliweza kuiamini fedha nyengine baada ya kuzowea sarafu zao.

https://p.dw.com/p/13coT
Alama ya sarafu ya euro na Umoja wa Ulaya.
Alama ya sarafu ya euro na Umoja wa Ulaya.Picha: picture-alliance/chromorange

Mara moja, Wataliana wakajikuta wanabadilisha mzigo wa Lire 25,000 kwa euro 12 na senti 91 tu, raia wa Finland aliyekuwa na Finnmark 25 zikabadilika na kuwa euro 3 na senti 88, huku Mjerumani aliyekuwa na Deutschmark 20 akijikuta sasa na euro 10 na senti 23. Uzoefu huu mpya wa sarafu ya euro ulikuwa kama hisabati ya kimazingaombwe, ingawa bado ni jambo lisilo jawabu ikiwa kuujenga umoja wa sarafu hii kwenyewe nako kulikuwa kwa mazingaombwe.

Mawazo na mikakati ya mwanzo ya kuwa na sarafu moja kwa bara zima la Ulaya ilianza tangu mwanzoni mwa miaka ya '60, ingawa shinikizo la kuitekeleza mikakati hiyo lilitoka nje, kama pale tarehe 15 Agosti mwaka 1971, rais wa wakati huo wa Marekani, Richard Nixon, aliposema kwamba sasa sarafu ya dola ingelikuwa ikibadilishwa kwa gharama inayokaribiana sana na dhahabu.

"Ilikuwa ni matokeo ya vita vya Vietnam na fedha zilizotumika kwenye vita hivyo, ambapo sio tu kwamba utawala wa Nixon ulitaka kuibadilisha thamani ya dola kwa dhahabu, bali pia ndani ya mwaka 1972, 1973 ukataka kuifanya hiyo kuwa ni kanuni katika taasisi za fedha. Mawaziri wa fedha wa Ujerumani na Ufaransa wa wakati huo, walikuwa wameshaamua tangu mwaka 1945 kwamba ili Bretton Woods kufanya kazi vyema, basi kanuni za umiliki wa fedha lazima ziwekwe upya, lakini hatukuwa bado tumeweza kufanikisha masuala yote ya Muungano wa Kiuchumi." Ndivyo anavyokumbuka kansela wa zamani wa Ujerumani, Helmut Schmidt.

Ni Kansela Schmidt ambaye wakati huo alikuwa ndiye waziri wa fedha wa Ujerumani. Mtu anaweza kufahamu haja kubwa iliyokuwapo kwanza ya kuyakusanya mataifa ya Ulaya kwenye umoja, kwani hadi mwaka 1972, ni mataifa sita tu ndiyo yaliyokuwa yamesaini mkataba wa Jumuiya ya Kiuchumi. Na hayo bado yalikuwa yana wasiwasi wa hatima ya kifedha ya sarafu zao, kama yangelijiingiza kwenye umoja wa kifedha. Hata hivyo, kikaanzishwa kitengo cha fedha ya Umoja wa Ulaya, kwa jina la European Curreny Unit.

Kansela wa zamani wa Ujerumani, Helmut Schmidt.
Kansela wa zamani wa Ujerumani, Helmut Schmidt.Picha: picture-alliance/rtn - radio t

Jambo la kwanza kutekelezwa na kitengo hiki, lilikuwa ni pendekezo la kuelekea sarafu ya pamoja, kwa kuanzia na wazo la kuwa na sarafu mbili zinazotumika kwa wakati mmoja ndani ya mataifa wanachama wa Jumuiya ya Uchumi ya Ulaya, moja ya kila taifa na nyengine ya pamoja.

Alikuwa ni Rais wa Kamisheni ya Ulaya katika mwaka 1998, Jacques Delors, aliyetandika misingi ya Umoja wa Kiuchumi na wa Kifedha wa Ulaya kwa kuanzisha benki kuu ya Ulaya. Na tangu hapo, hatua za kuelekea sarafu ya pamoja zikawa zinapigwa licha ya vikwazo kadhaa.

Katika siku yake ya kwanza kujaribiwa kutumika katika mataifa kumi na moja ya Ulaya, hapo tarehe 4 Januari 1999, euro moja ilikuwa na thamani ya dola moja na senti 18. Hilo likawatia wasiwasi wanasiasa na wataalamu wa uchumi kwamba euro imeanza kwa kupoteza thamani yake mbele ya dola. Oktoba mwaka 2000 ukawa mwaka mbaya zaidi, kwani euro ilikuwa na thamani ya senti 88 za dola ya Marekani.

Tahriri moja ya Deutsche Welle siku hiyo iliuliza ikiwa kweli wanasiasa na wanauchumi walifanya maamuzi sahihi ya kuanzisha sarafu ya euro. Hoja ilikuwa, masoko ya fedha na wawekezaji hawakuonesha imani yoyote kwa sarafu hiyo mpya.

Viongozi wakuu wa mataifa makuu ya Kanda ya Euro, Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel (kulia) na Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa.
Viongozi wakuu wa mataifa makuu ya Kanda ya Euro, Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel (kulia) na Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa.Picha: picture-alliance/dpa

Theo Waigel, alikuwa ni waziri wa fedha wa Ujerumani katika miaka ya '90, ambapo Ulaya ilikuwa inaelekea kwenye Umoja wa Sarafu ya Euro. Anasema kwamba miongoni mwa sababu za kukosekana kwa imani ya masoko katika sarafu ya euro, ilikuwa ni tafauti ya uchumi katika mataifa yaliyokuwa ni wanachama au yaliyoonesha nia ya kujiunga na sarafu hiyo, ikiwemo Ugiriki.

Na leo, miaka zaidi ya kumi baadaye, inafahamika kuwa matatizo yale yale yaliyokuwapo wakati sarafu hii inaanzishwa, yapo hivi sasa pia.

"Matatizo tuliyonayo ni ya kifedha kwa mataifa fulani, ambayo mwishoni mwa miaka ya '80 yalipitia kwenye mgogoro wa kiuchumi, au ambayo yamefanya makosa katika uchumi wake. Lakini hatuna tatizo la sarafu ya euro, isipokuwa matatizo ya nchi fulani tu." Anasema Wagel.

Kwa maneno mengine, hakuna mgogoro wa sarafu ya euro. Hata kama mataifa mengi kwenye kanda ya euro yanakabiliwa na matatizo ya madeni, yamejikuta yakiwa na thamani zaidi kwa sababu ya euro. Yameweza kuyakopesha makampuni mabilioni ya pesa za kuwekeza, yameweza kupata utaalamu wa nje, yameweza kuchota riba kutoka mataifa mengine. Hivi sasa euro inachukuwa nafasi ya pili baada ya dola katika kuwekwa kwenye akiba ya fedha za kigeni duniani. Na licha ya mgogoro uliopo, bado thamani ya euro mbele ya dola imetulia.

Mwandishi: Rolf Wenkel/DW
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Saumu Yusuf