Samia asema ni haki kwa vyama vya siasa kufanya mikutano
3 Januari 2023Ni tarehe 3, ya mwaka 2023 na Rais Samia Suluhu Hassan leo amekutana na viongozi wa vyama vya siasa, huku akiridhia mambo makuu matatu katika medani za siasa nchini Tanzania ambayo yalikuwa kilio kikubwa cha wanasiasa.
Katika mkutano huo, Rais Samia, ameruhusu rasmi mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, lakini akisisitiza zaidi siasa za kistaarabu na kuepuka kejeli na matusi.
''Kwa hiyo uwepo wangu leo mbele yenu ni kuja kutoa kuhusa, kuja kutangaza kwamba liletangazo la kuzuia mikutano ya adhara limeondoshwa.''
Mkutano huo wa leo umehudhuriwa na viongozi wote wa vyama 19 vya siasa, wakiwamo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho hapo awali, kilisusia mikutano ya serikali na hata Rais alipounda kikosi kazi cha kukusanya maoni kuhusu demokrasia na hali ya kisiasa.
Mchakato wa katiba mpya
Akizungumza katika mkutano huo Rais Samia Suluhu alisistiza kuwa, ameitisha mikutano hiyo kwani kuna masuala yaliyozungumzwa na bado hayajatolewa maamuzi na hivyo akasema ipo haja ya kufanya taifa liwe kitu kimoja na kuwepo na maridhiano, huku akisisitiza mfumo wa R4 ambazo ni, Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko Kujenga upya nchi . Na kuhusu Katiba Mpya Rais amesema:
''Nataka kuwaambia kwamba serikali inadhamiria kukwamua mchakato wa marekebisho ya katiba kwa jinsi tutakavyo kuja kukubaliana hapo mbele.''
Hii si mara ya kwanza kwa Rais Samia Suluhu Hassan kukutana na viongozi wa siasa nchini akiwa Ikulu, hata hivyo mkutano wa leo unatajwa kuwa wenye kuleta mwelekeo chanya na maridhiano ya kisiasa nchini .