Samia apokea ripoti ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi
21 Machi 2022Rais Samia amebainisha dhamira ya utawala wake kutaka kuwa na mazingira mazuri ya kuendesha shughuli za kisiasa nchini humo.
Rais Samia aliyekutana na kikosi kazi hicho, ikulu jijini Dar es salaam amesema ni matamanio yake kuona Tanzania inaendelea kuwa moja na salama bila kuwa na kundi litakalohisi kuachwa nyuma katika safari ya kufurahia demokrasia ya kweli.
Ripoti hiyo iliyotolewa na kikosi kazi kilichoundwa na yeye hivi karibuni kikiwajumuisha watu wa makundi mbalimbali, imeorodhesha mambo yanayogusua maeneo kama katiba mpya, utawala wa kisheria, tume huru ya uchaguzi, sheria na kanuni pamoja na utendaji jumla wa vyama vya siasa.
Rais amewataka wajumbe wa kikosi hicho kwenda kunoa bongo zaidi ili hatimaye kuwasilisha ripoti itakayojibu njia bora za kuzitafutia majawabu changamoto hizo, ambazo nyingine ameteka zitafutiwa ufumbuzi wake wa haraka hata kabla ya kufanyika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024.
Kuhusu hoja ya katiba mpya hoja ambayo katika siku za hivi karibuni imekuwa ikipata nguvu mpya kutoka kwa wachangiaji wake, Rais Samia hajaonyesha moja kwa moja kama suala hilo atalishughulikia lini, lakini amesema anaamini iwapo baadhi ya kero zitashughulikiwa ipasavyo huenda hata kiu ya katiba mpya ikapata mwarobaini wake.
Mwenyekiti wa kikosi kazi hicho, Profesa Rwekaza Mkandala aliibua hoja ya katiba mpya na kupendekeza mchakato wake uanze mara moja baada ya kukamilika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Kikosi kazi hicho, kinaundwa na mkusanyiko wa watu kutoka makindi mbalimbali na inaaminika huenda kikaendelea na kazi hiyo kwa muda mrefu. Chama kikuu cha upinzani Chadema ni baadhi ya makundi ambayo yalisusia kujumuishwa na Rais Samia amesema bado ataendelea na mazungumzo na makiundi ya namna hiyo ili hatimaye yajumuishwe.