SADC yawataka wanachama kujihadhari na corona
29 Januari 2021Kinashuhudiwa kiwango kikubwa hivi sasa katika ukanda huo, huku SADC ikiwataka viongozi kutunga sera na mikakati ya pamoja ili kudhibiti janga hilo.
Wito huo umetolewa na mwenyekiti wa jumuia hiyo ambae pia ni Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi, ikiwa tayari visa vya maambukizi katika ukanda huo vilivyorekodiwa katika wiki mbili za kwanza kwa mwezi Janury ni 346,010, sawa na asilimia 22 ya maambukizi yote katika eneo la ukanda huo tangu kuingia kwa virusi vya corona barani Afrika.
Katika hotuba yake ya kuzungumzia maambukizi mapya ya virusi vya corona, amesema asilimia hamsini ya maambukizi yote barani Afrika yapo katika ukanda wa SADC, hatua alioitaja kuzorotesha shughuli za kiuchumi na kijamii katika ukanda huo ulio Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Katika hotuba yake iliyo na kurasa mbili, mbali na kuwapongeza wakaazi wa ukanda huo kwa uvumilivu walioonesha katika kipindi chote ametoa wito wa haraka kwa viongozi wa mataifa hayo kutunga sera za pamoja na mikakati mipana katika kudhibiti janga la COVID-19 linaloutikisa uchumi wa dunia.
Wachambuzui wa masuala ya kidiplomasia wanasema madhara zaidi ikiwemo kupoteza nguvu kazi yanaendelea kushuhudiwa hivyo kuna haja ushirikiano wa dhati miongoni mwao. Saidi Msonga mchambuzi wa masuala ya diplomasia.
Wakati wito huo unatolewa, Tanzania imekuwa ikichukua mwelekeo wake katika kupambana na janga la virusi vya corona, hatua iliyomfanya mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani, WHO kanda ya Afrika Matshidiso Moeti kuwaambia waandishi wa bahari kuwa wanaanzisha tena mazungumzo na viongozi wa ngazi za juu wa taifa hilo kutoa ushirikiano na mataifa jirani katika kudhibiti maambukizi.
Baadhi ya wanasiasa wanasema utashi wa kisiasa katika utekelezaji wa mazungumzo unahitajika. Ado shaibu katibu mkuu wa chama cha upinzani ACT Wazalendo anasema.
Hakuna kiongozi yoyote nchini aliyetoka hadharani na kuthibitisha kuwepo kwa maambukizi ya virusi vya corona, licha ya viongozi kuendelea kutoa tahadhari dhidi ya janga hilo.
Mwandishi: Hawa Bihoga