SADC: Watu milioni 68 wanakabiliwa na athari za ukame
18 Agosti 2024Takribani watu milioni 68 walioko kusini mwa bara la Afrika wanakabiliwa na athari za hali ya El Nino iliyoangamiza mazao katika eneo hilo kutokana na ukame, hayo yamesemwa katika mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika jana mjini Harare nchini Zimbabwe.
Ukame ulioanza mapema mwaka huu umeyaharibu mazao na kuathiri uzalishaji wa mifugo na kusababisha upungufu mkubwa wa chakula na kudorora kwa uchumi kwa kiwango kikubwa.
Soma zaidi. Zambia yahitaji msaada kukabiliana na ukame
Wakuu wa nchi kutoka mataifa 16 ya Kusini mwa Afrika walikuwa wanakutana katika mji mkuu wa Zimbabwe, Harare, katika mkutano wa 44 wa Jumuiya ya Maendeleo (SADC) kujadili masuala ya kikanda ikiwa ni pamoja na usalama wa chakula.
Mataifa ya Zimbabwe, Zambia, na Malawi tayari yameshaitangaza hali hiyo kuwa ni janga la kitaifa, wakati mataifa ya Lesotho na Namibia yakitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa wa kupatiwa msaada wa kibinadamu.