SADC kutatua mzozo Madagascar
2 Juni 2012Viongozi wa mataifa 15 wanachama wa SADC wameamua kuwakutanisha mahasimu hao wawili ikiwa kama jitihada ya kusuluhisha mgogoro wa kisiasa unaokikabili kisiwa hicho kwa takribani miaka mitatu sasa.
Katika kauli ya pamoja iliyotolewa katika mkutano wa kilele wa jumuiya hiyo uliyofanyika katika mji mkuu wa Angola, Luanda, viongozi hao wamesema shabaha kuu ni kuandaa muongozo wa kumaliza mgogoro na kuweka mazingira mazuri ya kufanyika uchaguzi huru na wa haki.
Mgogoro katika kisiwa hicho kilicho katika Bahari ya Hindi ulizuka Machi 2009, pale Rajoelina alipomuondoa madarakani Ravalomanana kwa kusaidiwa na jeshi la taifa hilo.
Novemba mwaka jana vyama vikuu vya siasa kisiwani humo vilisaini makubaliano ya kuunda serikali ya mpito kuelekea uchaguzi mkuu ili kuweza kufanikisha uchaguzi mkuu mpya ambao unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu au mapema mwakani.
Makubaliano hayo yalipaswa kutoa fursa ya uhuru wa Rais Ravalomanana anayeishi uhamishoni nchini Afrika Kusini kurejea nchini humo. Lakini kiongozi huyo hajapewa fursa hiyo. Alihukumiwa kifungo mwaka 2010 akiwa nje kutokana na tuhuma ya mauwaji ya waandamanaji yanayodaiwa kufanywa na walinzi wake.
Hata hivyo, Ravalomanana amejaribu mara kadhaa kurejea nyumbani ambapo Januari jeshi la Madagascar liliuzingira uwanja wa ndege katika mji mkuu Antananarivo na kutoruhusu ndege iliyomsafirisha kiongozi huyo isitue.
Aidha baada ya mazungumzo yake na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa yaliyofanyika Mei, Rajoelina alisema ana matumaini kwamba uchaguzi utafanyika "haraka iwezekanavyo" lakini alikuwa na mashaka kuhusu kurejea kwa Ravalomanana, ingawa alisema yupo tayari tu kufanya makubaliano ya kisiasa.
Mwandishi: Sudi Mnette/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef