1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaRwanda

Rwanda yakanusha kuwafadhili waasi wa Burundi waliopo DRC

30 Desemba 2023

Rwanda imekanusha matamshi ya rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye, yaliyodai kuwa serikali mjini Kigali inawafadhili waasi wanaoendesha hujuma dhidi ya Burundi.

https://p.dw.com/p/4ajJ2
Ruanda l Präsident Paul Kagame
Rais wa Rwanda Paul KagamePicha: Dan Kitwood/POOLAFP

Waasi hao ni wa Red Tabara wanaoendesha hujuma dhidi ya Burundi kutokea ardhi ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Taarifa iliyotolewa Jumamosi na serikali ya Rwanda imesema matamshi hayo ya rais Ndayishimiye hayana ukweli na kwamba nchi hiyo haina mahusiano na kundi lolote la wabeba silaha linaloindama Burundi.

Siku ya Ijumaa, Rais Ndayishimiye aliituhumu Rwanda kuwasaidia kwa hali na mali waasi wa Red Tabara, tuhuma zinazozidisha uhasama kati ya mataifa hayo jirani na wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Soma pia: Ndayishimiye aituhumu Rwanda kuwaunga mkono waasi wa Burundi

Serikali mjini Kigali imekumbusha kuwa hivi karibuni, iliwakabidhi kwa Burundi wanamgambo walioingia Rwanda hii ikiwa kudhihirisha azma ya ushirikiano na jirani yake huku ikiwataka viongozi wa Bujumbura kuwasilisha malalamiko yao kwa njia za kidiplomasia ili yapatiwe suluhu la kirafiki.

Hata hivyo rais Ndayishimiye alielezea masikitiko yake kwamba juhudi zote za majadiliano na Rwanda juu ya swala hilo hazijazaa matunda.