1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rufaa ya Rais Jacob Zuma yakataliwa

Jane Nyingi24 Juni 2016

Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma amekataliwa rufaa yake ya kutaka kuizuia mahakama moja nchini humo kufufua mashataka kadhaa ya rushwa yanayomkabili.

https://p.dw.com/p/1JDJr
Südafrika Präsident Jacob Zuma
Picha: picture-alliance/dpa/N. Bothma

Uamuzi huo unamwongezea shinikizo rais Zuma baada ya mahakama ya kikatiba, kushikilia kuwa uamuzi wa kutupiliwa mbali mashtaka hayo haukuwa wa busara na unapaswa kutafakariwa upya.

Tangazo hilo ni pigo jingine kwa rais Zuma ambae amekuwa akikabiliwa na shinikizo za kumtaka ajiuzulu. Hatua hiyo inawadia huku zikiwa zimesalia wiki sita tu kabla ya kufanyika uchaguzi wa mabaraza ya miji. Chama tawala African National Congress(ANC) kinakabiliwa na upinzani mkali huku masaibu yanayomkabili rais Zuma yakitumiwa kama silaha ya kukiadhibu chama hicho. Mahakama siku ya Ijumaa ilisema Rais Zuma na mkurugenzi wa mashtaka ya umma Shaun Abrahams hawakuwa na sababu zenye uzito kuzuia kuendelea mashtaka hayo.

Hadi sasa haifahamiki iwapo wawili hao watawasilisha rufaa kufuatia uamuzi huo wa mahakama, lakini wachambuzi wa maswala ya kisiasa wamesema upo uwezekano wa kuwasilisha rufaa katika mahakama ya juu.Lakini Issac Khomo ambae pia ni mchambuzi wa maswala ya kisiasa nchini Afrika kusini ana maoni tofauti.

"Kutokana na uamuzi huu Jacob Zuma atapaswa kupelekwa mahakamani, ili kusikiliza kesi zinazomsibu. Kesi hii inatokana na ununuzi wa silaha uliofanyika zaidi ya miaka 10 iliyopita na kufuatiwa na tuhuma nyingi za rushwa na hata kupatwa na hatia". Khomo anaendelea kusema kwamba minongono iliyopo ni iwapo Zuma atapelekwa mahakamani.

Mwezi Aprili mwaka huu uchunguzi uliofanywa na serikali kuhusu ununuzi wa silaha hizo haukupata ushahaidi wowote wa visa vya ulaji rushwa au ubadhidhirifu wa mali ya umma,japo wakosoaji wa rais Zuma walisema ripoti hiyo ilinuia kumkinga. Kiongozi huyo wa Afrika kusini amekuwa akikabiliwa na kashfa moja baada ya nyingine, lakini ameweza kustahimili mawimbi hayo makali kutokana na kuungwa mkono na chama chake cha ANC ambacho kimekuwa madarakani tangu mwaka 1994. Lakini kashfa hizi huenda zikatishia kupoteza umaarufu chama tawala cha ANC? ni swali nilomuuliza Issac Khomo mchambuzi wa maswala ya kisiasa nchini Afrika kusini. "ANC ni zaidi ya mtu, Zuma anaweza kuitwa, kuhojiwa na kuondolewa madarakani kama alivyotolewa Thabo Mbeki. ANC haiwezi kuyumba kwasababu ya mtu mmoja."

Wafuasi wa chama cha ANC Afrika ya Kusini
Wafuasi wa chama cha ANC Afrika ya KusiniPicha: Reuters/M. Hutchings

Mwezi huo huo wa Aprili mwaka huu Rais Zuma alinusurika kura ya kutokuwa na imani nae bungeni baada ya kupuuza uamuzi wa mahakama ya kikatiba mwaka 2014, wa kurejesha dolla millioni 16 za serikali zilizotumika katika ukarabati wa makazi yake ya Nkandla. Zuma mwenye umri wa miaka 74 atakuwa anakamilisha mihula yake miwili ya uongozi mwaka 2019, lakini kuna uwezekano chama cha ANC kumtafuta mgombea mwingine wa urais kuchukua nafasi ya Zuma kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Mwandishi:Jane Nyingi

Mhariri:Yusuf Saumu