1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rousseff achaguliwa tena kuiongoza Brazil

Josephat Nyiro Charo27 Oktoba 2014

Rais wa Brazil Dilma Rousseff amepata ushindi mdogo katika duru ya pili ya uchaguzi iliyofanyika Jumapili (26.10.2014). Amesema kipaumbele kitakuwa kufanya mageuzi ya kisiasa kupitia mjadala wenye uwazi.

https://p.dw.com/p/1DcZA
Dilma Rousseff bleibt brasilianische Präsidentin
Dilma Rousseff (kulia, mbele) akipongezwa na rais wa zamani wa Brazil Luiz Inacio Lula da SilvaPicha: Reuters

Rais wa Brazil Dilma Rousseff ameshinda mhula wa pili kuiongoza Brazil, baada ya kupata ushindi mdogo katika duru ya pili ya uchaguzi iliyofanyika jana Jumapili. Bi Roussef amesema kipaumbele cha mhula wake wa mwisho kitakuwa kufanya mageuzi ya kisiasa kupitia mjadala wenye uwazi. Mpinzani wake Aecio Nevez amekubali kushindwa.

Baada ya asilimia 99 ya kura kuhesabiwa, matokeo yalimuonyesha bi Dilma Rousseff akimpita mpinzani wake kwa kura zaidi ya milioni tatu na kujishindia asilimia 51.6 ya kura zote zilizopigwa. Kitovu cha ufuasi wake kilikuwa kaskazini mwa nchi, lakini pia alifanikiwa kupata kura za kutosha kutoka kwa raia wa tabaka la kati katika mikoa tajiri ya Kusini Mashariki. Huu ni ushindi wa nne mfululizo wa chama chake cha wafanyakazi - PT.

Hali ya shamra shamra ilishuhudiwa miongoni mwa wafuasi wa chama hicho katika mji mkuu Brasilia na mikoani, huku baadhi wakijimwaga mitaani na kushangilia katika madirisha ya nyumba zao.

Kampeni za uchaguzi wa duru ya pili zilikuwa kali zaidi tangu kurejeshwa kwa mfumo wa demokrasia nchini Brazil. Uchaguzi huu ulichukuliwa kama nafasi ya wabrazil kukihukumu chama cha PT ambacho kimekuwa madarakani kwa miaka 12, dhidi ya ahadi za upinzani za hatua mpya zinazonuia kuuinua uchumi.

Rousseff aahidi kufanya mageuzi

Mhula wa kwanza wa rais Rousseff ulikabiliwa na kashfa za ufisadi, hususan ile iliyowahusisha wanasiasa wakuu wa chama chake katika ubadhirifu wa mabilioni ya dola kupitia shirika la mafuta linalomilikiwa na serikali, Petrobas.

Akiwahutubia wafuasi wake baada ya kutangazwa mshindi, Bi Dilma Rousseff aliahidi kuzifanyia kazi hitilafu za mhula wa kwanza. ''Kuchaguliwa tena kunaelezea matumaini, hususan ya kuboresha matendo ya wale waliokuwa katika nafasi za uongozi. Najua huo ndio ujumbe wanaoutuma wananchi wanapomchagua kiongozi kwa mhula wa pili. Hayo ndio nimeyasikia katika vituo vya kupigia kura. Hiyo ndio sababu nataka kuwa rais bora zaidi kuliko nilivyokuwa hadi leo''

Katika hotuba hiyo, rais Rousseff alisema pia kwamba atazingatia nidhamu katika masuala ya bajeti, na katika kukabiliana na mfumko wa bei.

Aécio Neves verliert Stichwahl um brasilianisches Präsidentenamt
Kiongozi wa upinzani, Aécio Neves, amekubali kushindwaPicha: Reuters

Kuchaguliwa tena kwa Bi Rousseff kunaibakisha Brazil katika mrengo wa kati kisiasa, kati ya nchi kama Venezuela na Argentina ambazo zinazingatia zaidi sera za kisoshalisti, na nchi za pwani ya magharibi ya Amerika kusini kama Chile na Colombia ambazo uchumi wake huria unakuwa kwa kasi zaidi.

Mgombea wa upinzani, Aecio Neves alikuwa ameahidi kuuboresha uchumi wa nchi kwa kuanzisha sera za biashara huria, bila kuachana na mipango ya kijamii ya chama cha wafanyakazi cha Bi Rousseff. Hata hivyo wafuasi wa chama hicho walitilia shaka ahadi zake, wakimshuku kuwa tajiri ambaye utawala wake ungejali zaidi maslahi ya watu wa tabaka la juu.

Siku za mwisho za kampeni zilishuhudia lugha kali na kuchafuliana majina miongoni mwa wagombea. Rousseff alimtuhumu Neves kuwa na sera za upendeleo, na kuwa aliwahi kumpiga mpenzi wake. Neves alijibu kwa kumwita Rousseff muongo na mshiriki katika kashfa ya ubadhirifu wa fedha za kampuni ya mafuta.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/DPAE

Mhariri:Josephat Charo