Rose ataka wachezaji wake kuwa makini dhidi ya Freiburg
1 Mei 2023Leipzig, chini ya kocha wa awali Domenico Tedesco, iliikandika Freiburg katika fainali ya msimu uliopita na sasa klabu zote hizo zinawania nafasi ya kufuzu michuano ya Klabu bingwa barani Ulaya.
Freiburg yenye alama 56, alama mbili mbele ya Leipzig, zinachuana tena Jumamosi ijayo katika pambano la Ligi Kuu ya Bundesliga.
Soma pia:Mbio za ubingwa wa Ujerumani zashika kasi
"Hii ni mechi muhimu, ni nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Ujerumani na timu zote zinawania nafasi ya kufika fainali. Sidhani kama ninahitaji kuchochea hisia, wachezaji wangu wana hamu ya kuingia uwanjani, kama tu ilivyo kwa Freiburg,” Rose ameuambia mkutano na waandishi wa habari leo Jumatatu.
Marco Rose mwenye umri wa miaka 46 na kocha wa zamani wa Borussia Dortmund na Borussia Mönchengladbach hajawahi kushinda kombe lolote akiwa Ujerumani na hii inachukuliwa nafasi ya kufanya hivyo.
Rose aliwahi kushinda mataji mawili ya Ligi Kuu ya Austria akiwa na klabu dada ya Leipzig ya Salzburg.
Soma pia: Leipzig yamsajili Seiwald kutoka Salzburg
RB Leipzig ndio mabingwa watetezi wa Kombe la Shirikisho la Ujerumani DFB Pokal baada ya kuifunga Freiburg kupitia mikwaju ya penalti.
Katika nusu fainali nyingine, VfB Stuttgart itamenyana na Eintracht Frankfurt katika uwanja wa Mercedes Benz Arena.
Droo hiyo ilifanyika katika jumba la Makumbusho la soka la Ujerumani mjini Dortmund.
Fainali itachezwa kazika uwanja wa Olympiastadion mjini Berlin mnamo Juni 3, mwaka 2023.