1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Roble ataka wabunge kulindwa kuelekea uchaguzi Somalia

27 Aprili 2022

Waziri Mkuu wa Somalia amewaomba wanajeshi wa Umoja wa Afrika kuwalinda wabunge wakati wanapochagua uongozi mpya wa taifa hilo. Polisi na maafisa wa ujasusi pia wameombwa kutojiingiza katika mchakato wa uchaguzi huo

https://p.dw.com/p/4AWCv
Somalia Mogadischu Premierminister Mohamed Hussein Roble
Picha: Sadak Mohamed/AA/picture alliance

Ombi la waziri mkuu huyo  linafuatia baada ya matukio mawili ya hivi karibuni ambapo maafisa usalama wa Somalia wanatuhumiwa kuyalenga kwa risasi magari ya wabunge wawili nje ya hoteli ambako wabunge wapya walikuwa wakiapishwa.

Ili kuzuia baadhi ya maafisa wa jeshi hilo kujihusisha na maswala ya siasa  waziri wa usalama wa nchi hiyo Abdillahi Mohamed Nur alimsimamisha kazi mkuu wa polisi Abdi Hassan Hijar.

soma zaidi: Ukosefu wa usalama waongezeka Somalia kuelekea uchaguzi

Uchaguzi wa Somalia umecheleweshwa kwa muda mrefu kutokana na sababu kadhaa zikiwemo mvutano wa madaraka kati ya Rais Mohamed Abdullahi Mohamed na Waziri Mkuu Mohamed Hussein Roble na mashambulio yanayofanywa na makundi yenye itikadi kali za kidini.

Hali ya wasiwasi bado inashuhudiwa Somalia

Somalia Mogadischu Parlament
Baadhi ya wabunge wa bunge la Somalia Picha: Sadak Mohamed/AA/picture alliance

Hata hivyo bado kumekuwa na hali ya wasiwasi Kutokana na hali mbaya ya usalama kuugubika  uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika mnamo Mei 17.

Mwaka uliopita mzozo wa kisiasa nchini Somalia ulisabisha mgawanyiko kati ya vikosi vya usalama ambapo makundi hasimu ya wanajeshi yalipigana mitaani na kuongeza mvutano unaosababisha hali mbaya ya usalama kuelekea uchaguzi.

Matatizo ya kisiasa nchini Somalia yaliongezeka pale Rais Mohamed Abdullahi Mohamed alipojaribu kuongeza muda wake kwa miaka miwili zaidi baada ya muhula wa miaka minne kumalizika, hatua ambayo ilipingwa na bunge.

Shirika la fedha IMF limesema Uchaguzi wa spika katika bunge na seneti ni wa hatua muhimu katika kuanzisha serikali mpya nchini Somalia,ikiwa nchi hiyo inataka kutaendelea kupokea fedha za msaada kutoka kwenye shirika hilo.

Chanzo: afp,ap