Ripoti ya UNESCO:Robo milioni ya watoto duniani wakosa elimu
23 Juni 2020Kulingana na makadirio ya shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO, takriban asilimia 90 ya vijana walioathiriwa zaidi ni kutoka katika nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara na Asia. Umasikini umetajwa kuwa ndio haswa unaoathiri fursa za elimu.
Ripoti hiyo pia imeeleza kwamba mamilioni ya wavulana na wasichana wanabaguliwa katika mifumo ya elimu kwa sababu ya asili zao au ulemavu walionao. Mkurugenzi Mkuu wa Unesco Audrey Azoulay amesema janga la corona limeathiri zaidi shughuli za elimu na kwamba tatizo hilo la kiafya linaweza kuwa chanzo cha kuwafanya watoto wengi wasirudi shuleni hasa wasichana kutoka familia masikini.
Ripoti hiyo ya UNESCO imebaini kuwa katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, watoto wenye ulemavu, kwa asilimia 19 wapo chini ya kiwango cha kuhudhuria masomo na kwamba katika mataifa 20 masikini, barani Afrika yaliyo Kusini mwa Jangwa la Sahara, wengi wa wasichana wa vijijini hawapati elimu ya shule ya sekondari.
UNESCO imesema kwenye ripoti yake kwamba kwa bahati mbaya, makundi yenye matatizo mbalimbali yanawekwa au yanasukumwa nje ya mifumo ya elimu kupitia maamuzi ambayo yanasababisha kutengwa kimitaala, malengo yasiyofaa katika ufundishaji, vitabu vinavyotumiwa, ubaguzi katika ugawaji wa rasilimali, vurugu na hata kupuuzwa kwa mahitaji ya wanafunzi.
Mkurugenzi Mkuu wa Unesco Audrey Azoulay amesema kwenye ripoti hiyo kwamba nchi nyingi bado zina matendo ya kuwabagua watoto kimasomo, ambayo yanachochea uhasama, ubaguzi na kutengwa.
Ameeleza kwamba ni nchi 41 tu ulimwenguni zinazotambua rasmi lugha ya ishara na kote ulimwenguni, shule nyingi zinang'ang'a pakubwa ya kuweza kupata huduma za inataneti kuliko kuwapa kipaumbele wanafunzi wenye ulemavu.
UNESCO inazihimiza nchi kuzingatia watoto walio kwenye mazingira magumu wakati shule zitakapofunguliwa tena baada ya kufungwa kwa sababu ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.
Azoulay amesema ili kuondokana na changamoto hii hoja ya kuwekeza elimu kwa kuwajumuisha wote bila ubaguzi ni muhimu zaidi na kwamba kushindwa kuchukua hatua endelevu ni kitendo kitakachozuia maendeleo kwa jamii.
Chanzo: AFP