Ripoti ya Marekani: Uturuki imepeleka wapiganaji Libya
18 Julai 2020Ripoti hiyo ni ya kwanza kutoa maelezo ya jinsi Uturuki inavyopeleka wapiganaji ambao wanajaribu kusaidia kubadilisha mkondo wa vita nchini Libya.
Ripoti hiyo inakuja wakati mzozo katika nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa mafuta unaongezeka na kuwa vita vya mataifa ya kigeni yanayopigana ndani ya nchi hiyo vita vinavyochochewa na mataifa hayo ya kigeni kwa kuingiza silaha na wapiganaji mamluki nchini Libya.
Jeshi la Marekani limekuwa na wasi wsi mkubwa juu ya ushawishi wa Urusi nchini Libya, ambako mamia ya wapiganaji mamluki wa Urusi wanaunga mkono kampeni ya kuukamata mji mkuu , Tripoli, upande wa magharibi ya nchi hiyo.
Ripoti hiyo ya robo mwaka kuhusu operesheni za kupambana na ugaidi katika bara la Afrika iliyotolewa na kitengo cha uangalizi cha wizara ya ulinzi, na kuchapishwa siku ya Alhamis, imesema Uturuki imelipa na kutoa uraia kwa maelfu ya wapiganaji mamluki wanaopigana pamoja na wanamgambo wenye makao yao mjini Tripoli dhidi ya vikosi vya kamanda aliyeko upande wa mashariki nchini Libya Khalifa Haftar.
Mafungamano na al-Qaeda
Licha ya ripoti zilizozagaa za mahusiano na wapiganaji wenye itikadi kali, ripoti hiyo inasema jeshi la Marekani halikupata ushahidi kuonesha kwamba wapiganaji hao mamluki wana mafungamano na kundi la itikadi kali linalojiita Dola la Kiislamu ama al-Qaida. Imesema ripoti hiyo kwamba kuna uwezekano mkubwa kuwa walihamasishwa na kiasi kikubwa cha fedha badala ya nadharia ama siasa.
Ripoti hiyo inajumuisha tu robo ya kwanza ya mwaka, hadi mwisho wa mwezi Machi, miezi miwili kabla ya mfululizo wa ushindi uliopata usaidizi kutoka Uturuki wa majeshi ya serikali ya Tripoli na kuyafurusha majeshi ya Haftar kutoka katika maeneo ya karibu na mji huo mkuu, katika ngome yake kuu ya Tarhuna na kituo kikuu cha jeshi la anga upande wa magharibi.
Kubadilishwa kwa mafanikio ya Haftar na waungaji wake mkono wa kigeni, ikiwa ni pamoja na Misri, Urusi na Umoja wa Falme za kiarabu, kumemulika uhusika unaoongezeka wa Uturuki katika vita hivyo vya mataifa ya nje ndani ya Libya.
Ripoti hiyo ya hivi karibuni inasema upelekaji wa majeshi unaofanywa na Uturuki huenda uliongezeka kabla ya ushindi wa majeshi ya serikali ya Tripoli mwishoni mwa mwezi Mei.
Inanukuu kamandi ya majeshi ya Marekani katika Afrika ikisema kuwa waasi 300 wa Syria waliokuwa wakisaidiwa na Uturuki waliwasili nchini Libya mapema mwezi Aprili. Uturuki pia iliweka "idadi isiyojulikana" ya wanajeshi wa Uturuki katika miezi ya mwanzo ya mwaka huu, mrakibu mkuu aliongeza.